TAKWIMU SAHIHI NI MSINGI WA UTEKELEZAJI BORA WA AFUA ZA NTD:DKT. MWANSASU:

 


Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTD) kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Clara Mwansasu, amesema kuwa utoaji wa takwimu sahihi na kwa wakati ni msingi muhimu wa utekelezaji bora wa afua za Magonjwa hayo  nchini.


Akizungumza Mkoani Morogoro katika kikao cha kuhuisha taarifa za Kadi ya Alama (Score Card) ya NTD kilichoratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na OWM -TAMISEMI na Muungano wa Viongozi wa Kupambana Malaria Afrika, African Leaders Malaria Alliance (ALMA), Dkt. Mwansasu amesema kuwa uboreshaji wa takwimu ni hatua muhimu katika kuongeza uwajibikaji na ufanisi wa utekelezaji wa afua za Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele nchini.


Amesema Kadi ya Alama ni nyenzo muhimu inayosaidia kuonesha hali halisi ya utekelezaji wa mipango katika mikoa, kubaini mafanikio pamoja na changamoto zilizopo, na kuweka mikakati ya maboresho kwa wakati.


“Utoaji wa takwimu kwa wakati utasaidia kwa kiwango kikubwa utekelezaji wa afua za Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele. 


Kadi ya Alama itatuonesha tulipo na namna gani ya kuongeza uwajibikaji katika kuboresha huduma,” amesema Dkt. Mwansasu.


Kwa upande wake, Afisa Mpango anayeratibu Ufuatiliaji, Tathmini na Tafiti kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, Dkt. Stephen Mbwambo, amesema kikao hicho kimewapa fursa waratibu wa NTD pamoja na waratibu wa takwimu za Afya ngazi ya mkoa (HMISFP) kujadili juu ya upatikanaji, uchakataji  na uhakiki ubora wa takwimu  ili kuhakikisha zinakuwa sahihi, kamili na zenye kuaminika katika kufanya maamuzi sahihi.


Ameeleza kuwa kupitia mchakato wa kuhuisha Kadi ya Alama, washiriki wameweza kubaini maeneo yanayohitaji kuimarishwa katika utoaji wa huduma za NTD, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo.


Mratibu wa NTD  Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI Dkt. Irene Haule  amesema kuhuisha takwimu za Kadi ya alama ni muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa kukabiliana na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele. 


Kikao hicho kimewakutanisha Waratibu wa Mikoa wa NTD na Maafisa Takwimu ngazi ya Mkoa kwa lengo la kujengewa uwezo wa matumizi ya takwimu katika kupanga, kufuatilia na kutathmini afua mbalimbali za magonjwa hayo.


Kupitia mafunzo hayo na uhuishaji wa Kadi ya Alama, washiriki wanatarajiwa kurejea katika mikoa yao wakiwa na uelewa mpana na uwezo wa kutumia takwimu kwa tija, hatua itakayochochea maboresho ya huduma na kuimarisha mapambano dhidi ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele nchini.







🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.
Previous Post Next Post