Na , Wellu Mtaki, Dodoma .📍
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili(MOI) Balozi Dkt Mpoki Ulisubisya amesema Taasisi hiyo kwa kipindi cha mwezi wa Kwanza mwaka 2025 imehudumia wagonjwa wa nje na wadharura 176,987 na wagonjwa wa ndani wakiwa 9,922.
Ameongeza kuwa huduma hizo zimefanikiwa kutokana na uwekezaji mkubwa ndani ya Taasisi hiyo kupitia serikali ya awamu ya Sita ambapo pia Mkurugenzi Mtendaji ameongeza kuwa Moi kwa Mwaka 2025 walianzisha huduma mpya 9 za kibobezi ambapo awali wagonjwa walikuwa wanapata huduma hizo kutoka nchi za nje.
Ameyasema hayo Wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma kuelezea mafanikio ya Taasisi hiyo pamoja na huduma zinazopatikana kwa ajili ya wananchi.
Balozi Dkt Mpoki amezitaja baadhi ya huduma hizo ikiwa ni pamoja na upasuaji wa ubongo kwa kutumia Akili Unde, upasuaji wa Mgongo kwa njia ya matundu, huduma ya kuchukua sampuli za vipimo kwa njia ya matundu, huduma ya kuweka tiba sementi kwenye pingili za mgongo zilizovunjika, huduma ya tiba ya maumivu, pamoja na huduma ya upasuaji rekebishi kwa viungo vilivyo pooza.
Aidha Balozi, Dkt Mpoki amebainisha kuwa Taasisi hiyo itaendelea kutekeleza kwa vitendo maagizo ya Serikali kwa kusogeza huduma za kibingwa na bobezi karibu na Wananchi kupitia huduma ya Tiba mkoba katika Hospitali mbalimbali ikiwemo Nyagao-Lindi , St Benedict- Ndanda, Hospitali ya Nkinga Tabora, Hospitali ya rufaa Chato pamoja na Tosamaganga Mkoani Iringa.

