VIJANA NCHINI WATAKIWA KULINDA AMANI NA KUEPUKA VURUGU


Mbunge wa Viti Maalumu kundi la Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Nyamizi Mhoja, ametoa wito kwa vijana nchini kulinda amani na kuepuka kushawishiwa kushiriki vitendo vya vurugu vinavyochochewa na makundi yenye nia mbaya dhidi ya taifa.


Akizungumza leo Februari 09,2026  wakati akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jijini Dodoma Mhe. Nyamizi amewahimiza vijana kushirikiana na wizara inayosimamia masuala yao ili waweze kunufaika na fursa zilizopo na kuchangia maendeleo ya taifa. 


"Tusijihusishe na makundi ambayo hayafai katika jamii, tuilinde nchi yetu vijana sisi ndiyo wenye hii nchi, tuepukane na vikundi hatarishi katika jamii na ndipo tuna uwezo wa kusema nchi itaendelea,"amesema. 


Amesema vijana wanapaswa kuwa sauti ya maendeleo ya taifa lao, hivyo amewaomba wasibweteke na wahakikishe wanaipambania nchi yao.


"Tuipambanie nchi yetu, tujiepushe na vitendo vya kiharifu vinavyoweza kuvunja amani ya nchi yetu, tujikite katika mambo ya maendeleo na sio vinginevyo, na bahati nzuri kwasasa tunayo Wizara inayoshughulikia mambo yetu vijana tuhakikishe tunaipa ushirikiano ili siku moja tunazungumzia maendeleo ya vijana tunaposhirikishwa tushiriki kikamilifu,"amesema. 


Katika hatua nyingine amewaomba vijana wawe wazalendo halisi kwa kuipenda nchi yao kutoka moyoni kwa kuilinda, kwani taifa lilivyo kwa sasa lilijengwa na vijana ambao ni wazee kwa sasa.

Previous Post Next Post