Timu ya Watalaam wa Ushirikishaji Jamii na Mawasiliano wakati wa Dharura kutoka Wizara ya Afya imefika katika Mkoa wa Tanga na Kuonana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Japhet Lazaro Simeo kwa ajili ya kujadili mikakati ya kuimarisha na kuboresha mbinu za Uhamasishaji na Ushirikishaji wa Jamii kujikinga na Ugonjwa wa Kipindupindu katika Wilaya ya Lushoto.
Dk.Simeo ameeleza jinsi jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali ya Mkoa katika kuhakikisha inakabiliana na mlipuko wa Ugonjwa huo.
Timu ya Wizara ya Afya inatarajia kuungana na Timu ya Mkoa wa Tanga ya Uhamasishaji na Ushirikishaji Jamii, pamoja na Timu ya Wilaya ya Lushoto katika kuyafikia makundi mbalimbali na kutoa Elimu kwa Jamii Jinsi ya kujikinga na mlipuko wa Ugonjwa wa kipindupindu pamoja na Magonjwa mengine.
Timu hizo kwa pamoja zikiwa katika Wilaya ya Lushoto, zinatarajia kufanya mafunzo kwa viongozi wa vijiji, watoa huduma za Afya ngazi ya jamii na makundi mengine ya watu maarufu katika jamii ili kusaidia katika kutoa elimu na kuhamasisha jamii katika kuchukua tahadhari ya kujikinga.



