NIT YAHAMASISHA WANAFUNZI SEKONDARI KUSOMA SAYANSI NA HISABATI

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Wanafunzi wa shule za sekondari nchini wametakiwa kuwa mstari wa mbele kuchangamkia masomo ya Sayansi na Hisabati na kuachana na dhana potofu kuwa masomo hayo ni magumu, huku wazazi na walezi wakisisitizwa kutowakatisha tamaa watoto wao ili kuwawezesha kupata ajira mara baada ya kuhitimu masomo.


Wito huo umetolewa leo Februari 23, 2026 jijini Dodoma na ujumbe wa wataalamu kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) walipotembelea shule za sekondari kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi kutokana na kukua kwa kasi kwa Sayansi na Teknolojia duniani.



Akizungumza katika ziara hiyo, Mhadhiri Msaidizi wa NIT, Bi. Doroth Manoza, amesema jamii imekuwa na mtazamo potofu juu ya somo la Hisabati kwa kuliona kuwa gumu, hali ambayo imechangia wanafunzi wengi kulikimbia.


“Hisabati ni somo kama masomo mengine. Mwanafunzi anaweza kufanikiwa kama anavyofanya katika masomo mengine. Changamoto kubwa mara nyingi ni misingi mibovu ya awali, hivyo wanafunzi wasikimbie somo hili bali wajitahidi kuimarisha misingi yao,” amesema.


Aidha, amewataka wazazi kuacha kuwakatisha tamaa watoto wao, hususan mabinti, kwa kuwazuia kuchagua masomo ya sayansi. 


Amesema bado kuna dhana potofu kuwa msichana akisoma sayansi au hisabati ataathiriwa katika maisha yake ya baadaye, jambo alilosisitiza kuwa si la kweli.


“Dunia ya sasa ni ya Sayansi na Teknolojia. Hakuna sababu ya mtoto, iwe wa kiume au wa kike, kuzuiwa kusoma masomo ya sayansi,” ameongeza.



Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa NIT, Bw. Juma Mandai, amesema kuna fursa nyingi za ajira katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji zinazohitaji wataalamu wa sayansi, hasa katika miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na serikali.


Amesema serikali inaendelea na mradi wa kufufua Shirika la Ndege la Taifa kwa kununua ndege za abiria na mizigo, ambazo zinahitaji wataalamu kama marubani na wahandisi wa ndege. 


Hata hivyo, amesema wataalamu hao bado ni wachache nchini, hali inayolazimisha serikali kutumia gharama kubwa kuajiri wataalamu kutoka nje.


“Tunawahitaji wataalamu wazawa ili kupunguza gharama na kuongeza ajira kwa vijana wetu. Vilevile kuna miradi ya ujenzi wa meli na maboresho katika sekta ya usafirishaji ambayo inahitaji wataalamu wa sayansi,” amesema.


Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Chinangali jijini Dodoma, walipozungumza kwa nyakati tofauti, wameeleza kufurahishwa na ziara ya wataalamu hao na kusema imewaongezea hamasa ya kujikita katika masomo ya sayansi.



Salim Hassan, mwanafunzi wa shule hiyo, amesema awali wanafunzi wengi walikuwa wanakimbilia masomo ya sanaa, lakini ujio wa NIT umebadilisha mtazamo wao.


“Tumejifunza kuwa ajira nyingi zipo kwenye fani za sayansi. Hasa wanafunzi wa kidato cha kwanza wamehamasika zaidi,” amesema.


Naye Sakina Mustafa amesema masomo ya sayansi si ya wavulana pekee bali hata wasichana wana uwezo wa kufanya vizuri na kufikia malengo yao.



Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Chinangali, Mwalimu Victor Salisali, amekiri kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa walimu wa sayansi, lakini akasisitiza kuwa hilo lisitumiwe kama sababu ya wanafunzi kukimbia masomo hayo.


“Sasa tupo kwenye zama za Sayansi na Teknolojia. Tumetoka kwenye mfumo wa analojia na sasa tupo kwenye mfumo wa kisasa zaidi. Wanafunzi wanapaswa kuendana na mabadiliko hayo kwa kujikita katika masomo ya sayansi,” amesema.


Uongozi wa NIT umeeleza kuwa utaendelea na ziara katika shule mbalimbali za sekondari kuanzia Februari 23 hadi 27, 2026, kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kuongeza ufaulu katika masomo ya sayansi na baadaye kujiunga na fani za sayansi katika elimu ya juu.







🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post