Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Serikali imewataka Watanzania kuchangamkia kikamilifu fursa za ufadhili wa masomo zinazotolewa ndani na nje ya nchi, ikibainisha kuwa kushindwa kuzitumia kunawaumiza wanafunzi wengine wanaotegemea kupata elimu kupitia mifumo ya ndani ya mikopo na rasilimali za Serikali.
Wito huo umetolewa leo Januari 20, 2025 jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, wakati wa kikao cha kimkakati cha Wizara hiyo kilichowakutanisha viongozi wa Wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake.
Prof. Mkenda amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha upatikanaji wa fursa za mikopo kwa wanafunzi wa ndani, hususan pale ambapo ufadhili wa asilimia 100 kutoka nje ya nchi unakuwa umetolewa lakini haukutumika ipasavyo kutokana na uzembe au ukosefu wa taarifa.
Amesisitiza kuwa hali hiyo inasababisha kunyimwa nafasi wanafunzi wengine wanaohitaji msaada wa kifedha.
Amesema kikao hicho ni muhimu kwani kinatoa fursa ya kutathmini utekelezaji wa bajeti ya nusu mwaka na kuweka vipaumbele vya mwaka wa fedha unaofuata, kwa kuzingatia malengo ya muda mfupi na mrefu ya sekta ya elimu.
Katika hatua nyingine, Prof. Mkenda amebainisha kuwa Serikali inalenga kutumia kikamilifu fursa za ufadhili wa masomo (scholarships) zinazotolewa na nchi rafiki na taasisi mbalimbali za kimataifa ili kupunguza utegemezi wa mikopo ya elimu ya juu na kuongeza idadi ya Watanzania wanaonufaika na elimu.
Ameeleza kuwa Tanzania imekuwa na changamoto ya kushindwa kutumia ipasavyo fursa nyingi za ufadhili wa nje kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi, uratibu dhaifu na mifumo isiyo imara ya ufuatiliaji. Kutokana na hilo, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha fursa hizo zinawafikia na kuwanufaisha Watanzania wengi zaidi.
Aidha, Prof. Mkenda amesema Serikali iko katika hatua za kuimarisha mfumo wa kitaifa wa takwimu za elimu utakaofuatilia mwenendo wa mwanafunzi kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu au mafunzo ya ufundi.
Amesema mfumo huo utawezesha upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazosaidia kupanga sera, bajeti na mipango ya maendeleo ya sekta ya elimu kwa ufanisi zaidi.
Ameongeza kuwa uwepo wa takwimu zisizo sahihi au zisizounganishwa umekuwa kikwazo kikubwa katika upangaji wa sera za muda mrefu, hivyo Wizara inalenga kuwa na mfumo mmoja unaounganisha taasisi zote za elimu, ikiwemo Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), NACTVET, vyuo vikuu na taasisi nyingine.
Kuhusu sera ya elimu, Prof. Mkenda amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka kumi, itakayohakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu hadi kidato cha nne bila kikwazo cha gharama, akisisitiza kuwa utekelezaji wake utahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Wizara, taasisi zake na wadau wa elimu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema kikao hicho ni jukwaa muhimu la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mwelekeo wa utekelezaji wa sera na mipango ya Wizara.
Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi, taasisi na wataalamu wa sekta ya elimu ili kuhakikisha mageuzi yanayopangwa yanatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa Taifa.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, alisema kikao cha nusu mwaka ni sehemu ya utaratibu wa Wizara wa kutathmini utekelezaji wa majukumu yake na kupanga kwa pamoja hatua za utekelezaji kwa kipindi kijacho.
Amesema kikao hicho kinajadili utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo iliyoboreshwa, masuala ya elimu kidijitali, utekelezaji wa bajeti pamoja na upatikanaji wa fursa za elimu na ufadhili wa elimu ya juu, akisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Wizara na taasisi zake ni msingi wa kufanikisha dira ya maendeleo ya Taifa kupitia sekta ya elimu.
🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya Washindi Media.





