KATIBU MKUU WA CCM AAGIZA VIONGOZI KURUDI MASHINANI KUTIMIZA AHADI NA KUIMARISHA MAENDELEO YA WANANCHI.


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Asha Rose Migiro, ametoa maagizo kwa viongozi wa chama katika ngazi zote kurejea mashina, matawi na kata ili kuimarisha utekelezaji wa ahadi za chama na kutatua changamoto za wananchi moja kwa moja.


Akizungumza leo Januari 20, 2026 katika mkutano wa mabalozi wa mashina wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Migiro amesema ushindi mkubwa uliofikiwa katika uchaguzi ni mwanzo wa kazi kubwa ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi, na akasisitiza kuwa utekelezaji huo lazima uanze mashinani.



“Tayari tumekamilisha uchaguzi na tumepata ushindi mnono. Kazi iliyopo sasa ni kuubadilisha ushindi huo kuwa utekelezaji wa ahadi na maendeleo kwa wananchi, na hilo litaanzia mashinani,” alisema Dkt. Migiro.


Katibu Mkuu huyo ameagiza viongozi ambao hawajafanya vikao vya mashina kuhakikisha wanakifanya mara kwa mara, akibainisha kuwa mashina ndiyo ngazi sahihi ya kubaini changamoto za wananchi na kuziwasilisha ngazi za juu kwa ufumbuzi.


Aidha, Dkt. Migiro amesisitiza kuwa mashina siyo jukwaa la wakereketwa pekee, bali ni fursa kwa wananchi wote, wanachama na wasiokuwa wanachama wa CCM, kujadili maendeleo ya jamii na masuala yanayohusu taifa.


Viongozi wanapaswa kutumia mashina kutangaza utekelezaji wa ilani ya CCM, kusikiliza kero za wananchi na kuzigeuza kuwa fursa za maendeleo, amesema Dkt. Migiro.


“Viongozi wetu wa juu warudi mashinani, tufanye vikao, tukusanye hoja na maoni, na tuyapeleke ngazi za juu. Hapo ndipo tutajenga chama chenye nguvu na taifa imara,” aliongeza.


Aidha, Dkt. Migiro ameeleza kuwa mashina ya CCM yawe ngome ya ulinzi wa chama na sehemu ya kuandaa viongozi wa baadaye, akisisitiza kuwa huko ndiko kunapoonekana kwa karibu mwenendo wa jamii na ulinzi wa maslahi ya taifa. Viongozi wanatakiwa pia kuunganisha maamuzi ya chama, kuwasilisha sera zinazounda mshikamano, na kutumia changamoto zilizopo kama fursa ya kuimarisha CCM.



Kwa upande wake, Mbunge wa Mtumba na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, akitoa shukrani kwa niaba ya wabunge waliokuwepo, amesema mabalozi wa mashina wamepokea maagizo hayo na wako tayari kuyatekeleza kwa vitendo kwa kushirikiana na wananchi.





🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya Washindi Media.

Previous Post Next Post