NDANI YA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA AJIRA 12,000 ZIMETOLEWA; ZAIDI YA WATUMISHI 8,000 WAMERIPOTI KAZINI

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍

Serikali imetoa kibali cha ajira kwa nafasi 12,000, zikiwemo ajira 7,000 za ualimu na ajira 5,000 za watumishi wa afya, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais ndani ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita.


Akizungumza na waandishi wa habari Januari 30, 2026  jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwan Kikwete, amesema kuwa kibali hicho cha ajira kilitolewa baada ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuapishwa tarehe 3 Novemba 2025.

Amebainisha kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 7, kifungu kidogo cha 7 cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, jukumu la kuendesha mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma linafanywa na Sekretarieti ya Ajira iliyo chini ya Ofisi ya Rais. Amesema kuwa baada ya tangazo la ajira kutolewa na maombi kupokelewa, Sekretarieti ya Ajira ya Utumishi wa Umma iliratibu usaili uliofanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na vituo maalum vya Unguja na Pemba.

Pia ameongeza kuwa usaili wa mchujo (Aptitude Test) ulifanyika kwa njia ya kidigitali kati ya tarehe 13–14 Desemba, na matokeo ya usaili huo yalitolewa siku hiyo hiyo. Amebainisha kuwa usaili wa mahojiano kwa waombaji wote waliofaulu usaili wa mchujo ulifanyika baadaye.


Amesema kuwa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma iliwapangia vituo wasailiwa wote waliofaulu kati ya  11–20 Januari, na barua za kupangiwa vituo zilitumwa moja kwa moja kwenye akaunti za waombaji badala ya utaratibu wa awali wa kufuata barua hizo jijini Dodoma.

‎Akizungumzia hatua ya uripoti, amesema kuwa hadi sasa jumla ya watumishi 8,416 wameripoti katika halmashauri mbalimbali nchini, wakiwemo watumishi 3,694 wa kada ya elimu na watumishi 4,722 wa kada ya afya.

Amebainisha kuwa kufuatia maelekezo ya  Rais Samia kuwa watumishi watakaoripoti mapema waingizwe kwenye orodha ya mishahara, watumishi 735 walioripoti kabla ya kufungwa kwa orodha ya mishahara waliingizwa kwenye payroll ya Serikali na tayari wamepata mishahara yao katika mwezi wa kwanza wa mwaka 2026.

Aidha, ameongeza kuwa bado watumishi 956 wa kada ya elimu pamoja na watumishi wa kada ya afya wapo kwenye mchakato wa kujaza nafasi zilizobaki, ambapo nafasi hizo tayari zimetangazwa na usaili unaendelea kufanyika. Amesema kuwa watumishi wote wataingizwa kwenye payroll ya Serikali kulingana na muda watakaoripoti katika vituo vyao vya kazi.

‎Aidha, ametoa maelekezo kwa  waajiriwa wapya wanapaswa kuripoti katika vituo vyao vya kazi ndani ya siku 14 tangu kupokea barua za kupangiwa vituo, na ameongeza kuwa wale watakaokiuka masharti hayo, nafasi zao zitachukuliwa na wasailiwa wengine waliobaki kwenye kanzidata.



🚨Full VIDEO Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.
Previous Post Next Post