WAZIRI MAVUNDE AAMURU KUFUTWA KWA LESENI 73 ZA MADINI ZISIZOENDELEZWA

 

Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameagiza Tume ya Madini kuchukua hatua za haraka kufuta leseni 73 za madini zinazomilikiwa na watu binafsi na kampuni ambazo zimedorora bila kuendelezwa kwa mujibu wa sheria na masharti ya utoaji leseni hizo.


Akizungumza jana jijini Dodoma mbele ya waandishi wa habari, Mavunde amesema Serikali imefikia hatua hiyo kutokana na kuchoshwa na tabia ya baadhi ya wawekezaji kuchukua leseni na kuzihodhi kwa miaka mingi bila kuanzisha shughuli zozote za uchimbaji, hali inayokwamisha maendeleo ya sekta ya madini pamoja na ukuaji wa uchumi wa taifa.


“Nimeielekeza Tume ya Madini kufuta mara moja leseni 73 ambazo hazina maendeleo yoyote. Sitavumilia watu au wawekezaji wanaochukua leseni na kuzifungia chumbani. Leseni si pambo. Ukichukua leseni lazima uende ukachimbe,” alisema kwa msisitizo.


Amebainisha kuwa wamiliki wa leseni hizo wamekuwa wakikiuka masharti muhimu ya kisheria, ikiwemo kutowasilisha mipango ya maendeleo ya miradi yao, kushindwa kutimiza masharti ya kifedha, kutokuanzisha shughuli za utafiti au uchimbaji, pamoja na kuhodhi maeneo bila sababu za msingi.


“Huu ni uzembe na kikwazo katika kuongeza mapato ya Serikali, ajira kwa Watanzania na kuendeleza mnyororo wa thamani wa madini. Tume ichukue hatua, sheria ichukue mkondo wake,” amesisitiza Mavunde.


Kwa mujibu wa waziri huyo, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na mifumo ya utoaji leseni, hatua iliyosababisha ongezeko la maombi mapya ya leseni za madini. Hata hivyo, alisisitiza kuwa ongezeko hilo haliwezi kuwa sababu ya kuvumilia wamiliki ambao hawatimizi wajibu wao.



Mavunde aliwataka wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo kuhakikisha wanafuata masharti ya leseni zao, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua zaidi ikiwa ni pamoja na kufuta leseni nyingine zitakazobainika kukiuka sheria.


“Kila anayemiliki leseni lazima afuate sheria. Tunataka sekta ya madini iwe na tija, iwe na matokeo na iwe na mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa,” amesema.


Kufutwa kwa leseni hizo 73 kunatarajiwa kufungua fursa mpya kwa wawekezaji wenye uwezo na nia ya kweli ya kuwekeza na kuendeleza maeneo ya madini yaliyokwama kwa muda mrefu.


Ikumbukwe kuwa Aprili 2025, Wizara ya Madini ilitangaza msako maalum wa leseni zisizoendelezwa na kutoa hati za makosa kwa kampuni mbalimbali, hasa kubwa, ambazo zilikuwa hazijaanza utekelezaji wa miradi yao. Baada ya hatua hiyo, baadhi ya kampuni ziliwasilisha utetezi wao na nyingine zikaanza rasmi shughuli za uchimbaji.






🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post