MKUU WA MKOA SENYAMULE AITISHA MAOMBI YA PAMOJA KUIMARISHA AMANI DODOMA.

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, leo Novemba 25, 2025 amekutana na waandishi wa habari jijini Dodoma na kueleza sababu ya serikali kukutana na viongozi wa dini ili kujadili kwa kina mustakabali wa amani ya mkoa huo muhimu kwa taifa.


Amesema serikali imeona umuhimu wa kuzungumza moja kwa moja na viongozi wa dini kwa kuwa wao wanafikia kundi kubwa la wananchi kupitia waumini wao, hivyo kuwa lango muhimu la kusambaza ujumbe wa kuimarisha na kutunza amani.


“Tumekutana na viongozi wa dini kwa sababu tunatamani kuona mkoa wa Dodoma unaendelea kuwa na amani wakati wote. Tunajua sisi tunawaita wananchi, lakini kwa upande wao wanaitwa waumini, kwa hiyo ni nafasi nzuri ya kufikisha lugha moja kuhusu umuhimu wa amani,” amesema Senyamule.


Amewashukuru wananchi wa Dodoma na viongozi wa dini kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha hasa katika kipindi cha uchaguzi uliopita ambapo mkoa uliendelea kuwa na utulivu. 


Amesema malengo ya serikali na maendeleo makubwa yanayopangwa katika Makao Makuu ya Nchi hayawezi kutimia bila amani ya kudumu.


Katika kikao hicho, viongozi wa dini kwa umoja wao wameahidi kuendelea kuhubiri amani katika nyumba zao za ibada, huku kila mmoja akionesha dhamira na utashi wa kutunza mshikamano wa jamii. Pamoja, wamekubaliana kuandaa maombi maalum ya pamoja yenye vipaumbele vitatu muhimu:


  1. Kumshukuru Mungu kwa mkoa kuendelea kustawi na kuvuka salama tarehe 29 na nyakati nyingine muhimu.
  2. Kuomba rehema, pamoja na kuendelea kuliombea taifa na mkoa ulinzi na neema.
  3. Kuomba amani endelevu kwa Dodoma, hasa ikizingatiwa kuwa ndiyo Makao Makuu ya Nchi na kitovu cha mipango mikubwa ya maendeleo ya serikali.

Mhe. Senyamule ameeleza kuwa timu ndogo imeachwa kuratibu utaratibu wa maombi hayo, ikiwemo tarehe na mahali ambapo yatafanyika, na taarifa rasmi zitatolewa mara baada ya maandalizi kukamilika. Ameeleza kuwa dhamira ya serikali ni kuona kila mwananchi wa Dodoma anashiriki siku hiyo muhimu ya maombi.


Akimazia, Mkuu wa Mkoa ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi wote wa Dodoma kuhakikisha wanaendelea kuilinda amani ya mkoa.


“Amani ya mkoa wetu ndiyo mustakabali wa maendeleo ya Dodoma. Naomba kila mwananchi aendelee kuithamini na kuilinda,” alisema.


🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post