UTT AMIS YAHIMIZA WATANZANIA KUACHA KUHIFADHI FEDHA BILA TIJA, WAWEKEZE KATIKA MIFUKO YA UWEKEZAJI

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Katika kuelekea kujenga taifa lenye uchumi imara na wananchi wenye uhuru wa kifedha, UTT Asset Management and Investor Services (UTT AMIS) imeendelea kutoa wito kwa Watanzania kuacha desturi ya kuhifadhi fedha bila tija na badala yake kuzielekeza kwenye uwekezaji wenye faida.


Akizungumza katika Maonesho ya Mat Builders & Contractors Global Expo 2025 yanayoendelea jijini Dodoma, Afisa Masoko wa UTT AMIS, Pascazia Charles, amesema kuwa ni muhimu kwa Watanzania kubadili mtazamo na kuanza kuiona fedha kama mbegu inayoweza kukua na kuzalisha zaidi iwapo itawekezwa ipasavyo.


“Hamasa kubwa ni kuwaelimisha Watanzania kutoka kwenye tabia ya kuweka tu pesa ndani au katika maeneo yasiyoleta faida. Tunataka watu waanze kuwekeza ili fedha iwe mbegu inayoanza kuchipua na hatimaye kukua,” alisema Pascazia.



Amefafanua kuwa uwekezaji ni sehemu muhimu ya kujijengea kipato cha kudumu, na kwa mtu anayeanza leo na kuendelea kwa muda mrefu, manufaa yake ni makubwa sana kiuchumi.


“UTT AMIS tunashiriki maonesho haya tukilenga kuwafikia wahandisi, wachimbaji wadogo wa madini, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla ili tuwape elimu sahihi ya uwekezaji,” aliongeza.


Pascazia amesema kuwa UTT AMIS ni taasisi ya serikali chini ya Wizara ya Fedha inayojihusisha na uwekezaji wa pamoja kwa kukusanya fedha kutoka kwa watu binafsi, vikundi, taasisi, SACCOS na makundi mengine. Hadi sasa inaendesha mifuko sita ya uwekezaji ambayo ni: Mfuko wa Umoja, Wekeza Maisha, Mfuko wa Watoto, Mfuko wa Kujikimu, Mfuko wa Ukwasi na Mfuko wa Hatifungani.


“Mifuko hii ina malengo tofauti ili kukidhi hitaji la kila mwekezaji. Tunatoa wito kwa wafanyabiashara, kampuni na vikundi kufungua akaunti za uwekezaji kwani tumetoa faida nzuri kwa miaka mitano mfululizo si chini ya asilimia 12,” alisema.



Kwa upande wake, Dorice Mlenge ambaye pia nia Afisa Masoko wa UTT AMIS, alibainisha kuwa taasisi hiyo inaendelea kutoa elimu kwa Watanzania kutofautisha kati ya kuweka na kuwekeza.


“Kuweka fedha unairudia vile vile, lakini ukifanya uwekezaji fedha inaongezeka. Tunataka Watanzania waiache pesa ifanye kazi na kuwazalishia,” alisema Dorice.


Ameeleza pia uwepo wa mfuko wa bond unaotoa gawio kila mwezi au kila miezi sita, na Mfuko wa Toto unaoruhusu uwekezaji kuanzia shilingi elfu 10 kwa ajili ya watoto na wajukuu.


Ametaja maeneo wanayopatikana kuwa ni Dodoma (Jengo la PSSF, ghorofa ya 6), Dar es Salaam (Jengo la Sukari), Mbeya, Zanzibar, Kahama na Morogoro.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha, alipotembelea banda la UTT AMIS ameonesha kufurahishwa na huduma za taasisi hiyo, akijivunia kuwa mwekezaji wa Mfuko wa Ukwasi.



Naye mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha alipotembelea banda la UTT AMIS katika maonesho hayo amesema, “Mimi ni muwekezaji wa ukwasi, na nataka kuwaambia wananchi ni vizuri kuwekeza UTT AMIS. Unapoweka fedha zako, zinakuzalishia faida kila siku. Huu ni kama nyumba inayotembea; unapata ‘kodi’ kila jioni,” alisema Mhe. Macha.


Ameitaka UTT AMIS kuongeza jitihada za kujitangaza zaidi nchini kwani watu wengi bado hawajui fursa hizo.
“Ninajuta kwa nini sikulijua hili miaka mingi iliyopita,” alisema huku akiipongeza taasisi hiyo kwa kuwafungulia wananchi milango ya uwekezaji salama na wenye tija.








🚨Full VIDEO inapatikana kwenye Instagram Page yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post