MUSLIM SISTERS FOUNDATION YAGUSA MIOYO HOSPITALI YA RUFAA DODOMA.


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Katika hatua ya kuimarisha mshikamano na huruma ndani ya jamii, taasisi ya Muslim Sisters Foundation (MSF) leo imefanya tukio la kipekee la kurudisha kwa jamii kwa kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, wakiianza rasmi safari yao ya huduma kwa jamii tangu kuzinduliwa kwao jijini Dodoma.


Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi na Mbeba Maono wa Muslim Sisters Foundation, Bi. Warda, alisema kuwa siku ya leo imebeba furaha na matumaini makubwa kwao kama taasisi.

“Najisikia furaha sana. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuongoza na kutuwezesha kufika hatua hii. 


Tulianza kama maono, kama dhamira, lakini tunaona jinsi Waislamu walivyoguswa na kutuunga mkono. Leo tumefika hospitali kuwajulia hali watoto na kushirikiana kufanya jambo linaloigusa jamii yetu,” alisema.



Bi. Warda aliongeza kuwa ziara ya leo ambayo ilijikita katika wodi za watoto ni mwanzo tu, na kwamba MSF imepanga kurejea hospitalini mara kwa mara mpaka watakapozifikia wodi zote.


“Huu ni mwanzo. Baada ya hapa tutapanga upya na kuhakikisha tunawafikia wagonjwa wote kwenye wodi zote,” alisisitiza.


Taasisi ya Muslim Sisters Foundation inajikita katika kuwaunganisha Waislamu na kuchochea utamaduni wa kusaidiana ili kuboresha ustawi wa jamii nzima bila ubaguzi.


“Tunamkaribisha mtu yeyote mwenye nia njema. Tunacholenga ni jamii yetu. Naomba jamii ijiandae na mwezi wa Ramadhani kwani mwezi wa pili tuna jambo kubwa kwa ajili ya jamii,” aliongeza Bi. Warda.



Kwa upande wake, mmoja wa wanachama wa taasisi hiyo, Bi. Hadija, alieleza jinsi ziara hiyo ilivyogusa hisia zake kama mama na mlezi.


“Ukiingia wodi ya watoto lazima uguswe. Watoto wanaumwa sana, maradhi ni mengi na mengine hatujawahi kuyaona. Wanahitaji msaada wetu — wazazi wao hawawezi kubeba mzigo huu peke yao,”alisema.


Bi. Hadija aliitaka jamii kujitoa kwa hali na mali, akisisitiza kuwa hata mchango mdogo kama sabuni unaweza kubadili hali ya mtoto.


“Tujitahidi kutoa chochote tulichonacho. Hawa watoto wanahitaji dua zetu, fedha na vifaa mbalimbali,”aliomba.


Ziara hii ya Muslim Sisters Foundation imeacha alama ya matumaini, ikionyesha uthibitisho kuwa jamii inapoungana, kila kilio kinaweza kubadilishwa kuwa tabasamu.











🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post