TANROADS YAHIMIZA UIMARA WA BARABARA KUKABILIANA NA ATHARI ZA MVUA


Mbande, Dodoma.📍


Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imewahakikishia wananchi kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua za haraka na za kitaalamu kuhakikisha huduma za usafiri na usafirishaji hazikatizwi na mvua zinazoendelea kunyesha nchini, hasa katika maeneo yaliyoathirika na changamoto za kimazingira.


Akizungumza leo Jumamosi, Novemba 22, 2025 katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na changamoto za mvua, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema serikali imeongeza nguvu katika kuboresha na kuimarisha miundombinu ya barabara ili kupunguza athari zinazoweza kutokea kutokana na mvua za msimu.


Ziara hiyo ilifanyika Mbande, wilayani Kongwa mkoani Dodoma, katika eneo ambalo kwa kipindi kirefu limekuwa likikumbwa na uharibifu kila msimu wa mvua. 


TANROADS imekamilisha uboreshaji wa kipande hicho cha barabara, na kwa sasa mradi upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.


“Hivi sasa hakuna tena changamoto katika eneo la Mbande. Tumeboresha miundombinu ili kuhakikisha mvua haziathiri tena barabara hii,” amesema Mhandisi Besta.




Akitaja maeneo mengine yaliyoathirika na mvua, amesema baadhi ya barabara katika mikoa ya Njombe ikiwemo barabara ya Itoni - Lusitu - Ruvuma, Mbeya, Arusha, Rukwa na Katavi zimepata madhara, huku sehemu nyingine zikipata changamoto kutokana na ujenzi unaoendelea.


Ameeleza kuwa TANROADS inaendelea kufanya kazi kwa kuzingatia Emergency Response Manual, mwongozo maalumu unaoelekeza hatua za kitaalamu za kuchukua wakati wa dharura zinazosababishwa na mazingira.


Katika msisitizo wake, Mhandisi Besta amewataka Mameneja wa TANROADS wa mikoa yote nchini kusimamia kwa umakini miradi na maeneo yao, si tu pale yanapopata athari za mvua, bali hata maeneo ambayo hayajaathirika ili kudhibiti uharibifu.








🚨Full VIDEO inapatikana kwenye Instagram Page yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post