Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza kukamilishwa kwa miradi ya maboresho ya miundombinu ya madaraja, barabara na maeneo ya maegesho wilayani Kongwa, mkoani Dodoma, ndani ya kipindi kisichozidi majuma mawili ili kuwanusuru watumiaji wa barabara na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Ulega ametoa maagizo hayo leo Novemba 22,2025 jijini Dodoma alipotembelea miradi ya maendeleo katika maeneo korofi ya Barqbara, ikiwemo Daraja na Tuta la Mbande, Mradi wa Dharura wa Ujenzi wa Madaraja na Tuta la Mtanana, Maegesho ya Magari Kibaigwa, pamoja na Mradi wa Dharura wa Ujenzi wa Madaraja na Tuta la Pandambili na Silwa.
“Jitahidini kutunza miundombinu. Yale yaliyotokea karibuni yametuchafua, na mna uwezo wa kufikisha changamoto zenu kupitia viongozi wenu. Serikali ipo tayari kusikiliza na kuzitatua. Msikubali kushawishiwa kufanya uharibifu,” amesema Ulega.
Aidha, Waziri Ulega amewataka wakandarasi wazawa wanaotekeleza miradi hiyo kufanya kazi kwa ubora, kasi na kwa kuzingatia viwango, akisema serikali ina maelekezo mahsusi ya kuwapa kazi wakandarasi waliothibitisha uwezo na uadilifu.
“Eneo hili lilikuwa na makaravati ya chuma ambayo hayakuweza kuchukua wingi wa maji. Tumeongeza makaravati mapya na kuinua tuta la barabara kwa urefu wa kilomita 2.5, pamoja na kurudishia matabaka ya barabara hadi kufikia hatua ya kuweka lami,” amesema.
Amesema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi mzawa King’s Builders LTD, uliyoanza Novemba 15, 2024 na unatarajiwa kukamilika Desemba 25, 2025 kwa gharama ya shilingi bilioni 7.9, fedha za dharura za SEC chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.
Mhandisi Zuhura amebainisha kuwa kuchelewa kupatikana kwa lami kulisababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli kwa takribani mwezi mmoja, lakini sasa ugumu huo umeondoka, na mkandarasi ameahidi kukamilisha kazi ya lami ndani ya wiki moja.











