UCHAGUZI HALALI KWA MUJIBU WA KATIBA – MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari (MB), amewahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika kesho ni halali na uko kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akisisitiza kuwa hakuna sababu yoyote ya kikatiba inayoweza kuzuia kufanyika kwake.


Akizungumza leo jijini Dodoma, Mhe. Johari amesema kuwa Ibara ya 5(1) ya Katiba inatoa haki kwa kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 kupiga kura katika uchaguzi unaofanywa na wananchi, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kutumia haki hiyo ya kikatiba.


“Wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote ya nchi yetu, na serikali hupata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba,” alisema Mhe. Johari akirejea Ibara ya 8(1)(a) ya Katiba.


Amesema kwa mujibu wa Ibara ya 42(2) na 65(1) ya Katiba, pamoja na Kifungu cha 56(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, uchaguzi mkuu hufanyika kila baada ya miaka mitano, na muda huo umeshakamilika kikatiba.





Aidha, Mhe. Johari alibainisha kuwa Katiba inatoa sababu chache sana zinazoweza kusababisha uchaguzi kusogezwa mbele, ikiwemo wakati ambapo nchi ipo vitani au endapo kutatokea kifo au kukosekana kwa wagombea. Hata hivyo, alieleza kuwa kwa sasa hakuna hali yoyote kati ya hizo mbili iliyopo nchini.


“Wale waliokuwa na mawazo ya kusogezwa mbele kwa uchaguzi huu walikuwa wanataka kuvunja Katiba yetu. Mawazo hayo hayana msingi wa kisheria na yanapaswa kupuuzwa,” alisisitiza.


Mhe. Johari aliwataka wananchi wote kutambua kuwa wagombea wa nafasi ya Urais, Ubunge na Udiwani wamepatikana kwa mujibu wa Katiba na Sheria, hivyo uchaguzi wa kesho ni halali na unafuata misingi ya kidemokrasia na utawala wa sheria.

“Naomba wananchi wote washiriki kikamilifu katika uchaguzi huu, kwani huu ni wajibu wa kikatiba na kiuzalendo,” aliongeza.


Aidha, Mwanasheria Mkuu alionya dhidi ya vitendo vya vurugu, vitisho au hila vinavyoweza kuwazuia wapiga kura kutumia haki yao ya kupiga kura, akieleza kuwa vitendo hivyo ni kosa kwa mujibu wa Kifungu cha 129 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.


“Mtu yeyote atakayejihusisha na kutumia nguvu, vitisho au hila kumzuia mpiga kura asipige kura, anatenda kosa la ushawishi mbaya. Sheria itachukua mkondo wake,” alisema kwa msisitizo.


Mwisho wa hotuba yake, Mhe. Johari aliwataka Watanzania kudumisha amani, umoja na utulivu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi, akisema kuwa misingi hiyo ndiyo uti wa mgongo wa demokrasia nchini.






🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post