JENESTA MALINGO AFUNGA KAMPENI KWA KISHINDO ZUZU, AHIMIZA AMANI NA USHIRIKIANO


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Mgombea wa Udiwani Kata ya Zuzu, Bi Jenesta Project Malingo, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amehitimisha rasmi kampeni zake kwa kishindo katika mkutano uliofurika wananchi wa kata hiyo, akiwataka wakazi wa Zuzu kujitokeza kwa wingi kesho asubuhi kupiga kura kwa amani na utulivu.


Akizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni uliofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Zuzu, Bi Jenesta amewataka wananchi kuamka mapema na kushiriki zoezi la kupiga kura kuanzia saa 1:00 hadi saa 10:00 jioni, huku akisisitiza kuwa hali ya amani na usalama iko imara katika kata hiyo.


“Ndugu zangu wana Zuzu, asubuhi tujikite kupiga kura. Mama usimuache baba, na watoto waliokomaa kupiga kura waende wakachague Chama Cha Mapinduzi. 


Amani ipo ya kutosha, usalama upo, asitokee mtu wa kututisha,” alisema Bi Jenesta kwa msisitizo, akipigiwa makofi na wananchi.


Bi Jenesta ambaye alikuwa Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) kata ya Zuzu kabla ya kuwania nafasi hiyo, amewashukuru wananchi kwa ushirikiano waliompa tangu kuanza kwa kampeni tarehe 28 Agosti 2025.



Amesema kampeni za CCM zimekuwa za amani, upendo na zinazolenga kuwaletea wananchi maendeleo yenye kasi, mshikamano na ushirikishwaji, ambayo ndiyo kauli mbiu yake katika uchaguzi huu.


Akielezea mafanikio yaliyopatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Jenesta ametaja miradi mikubwa iliyotekelezwa katika kata hiyo ikiwemo Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), barabara ya mzunguko (Ring Road), pamoja na uanzishwaji wa shule ya kidato cha tano na sita.


“Mama Samia ametuletea maendeleo tunayoyaona kwa macho yetu. Tumepata miradi mikubwa ya kimkakati, maji, umeme, na elimu. Kwa hilo, naomba kura za kutosha kwa ajili yake katika nafasi ya Urais, kwa Mbunge wetu Pascal Chinyele, na mimi Jenesta Malingo katika Udiwani,” alisema.



Kwa upande wake, Samuel Marwa Kisaro, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Dodoma Mjini) ambaye alikuwa mgeni rasmi, amewataka wakazi wa Zuzu kudumisha amani wakati wa uchaguzi na kuendelea kuamini katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030.


“Ilani yetu imeeleza wazi miradi mikubwa ya maji, elimu na barabara itakayotekelezwa hapa Zuzu. Hivyo, ni muhimu tumpe kura Dkt. Samia, Mbunge Chinyele, na Diwani Jenesta ili tuweze kusonga mbele pamoja,” alisema Kisaro.



Naye Mwenyekiti wa CCM Kata ya Zuzu, Omari Bilali Kagusa, aliwataka vijana kujiepusha na vurugu au maandamano, akisisitiza kwamba uchaguzi ni fursa ya kuimarisha umoja na siyo migawanyiko.


“Vijana wangu epukeni vurugu. Kesho nendeni mkapige kura, kisha mrudi nyumbani kupumzika. Tuvune ushindi kwa amani,” alisema Kagusa.


Wananchi wa Zuzu waliomaliza mkutano huo kwa nyimbo na nderemo, wakiahidi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa chama chao, huku wakimpongeza Bi Jenesta kwa kampeni zenye maono na umakini.


Kauli mbiu ya Jenesta Malingo:
“Maendeleo yenye kasi, mshikamano na ushirikishwaji wa wananchi.”












🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post