SERIKALI YAHAKIKISHA KIWANDA CHA KATUMBA NA MWAKALELI KUFUNGULIWA UPYA NDANI YA MIEZI MITATU

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Serikali imethibitisha kuwa Kiwanda cha Katumba na Mwakaleli kilichopo wilayani Rungwe, mkoani Mbeya, kitafunguliwa tena ndani ya miezi mitatu ijayo ili kuhakikisha wakulima wa chai wanaendelea kuuza mazao yao kama kawaida, huku wafanyakazi wote waliokuwa wamesimamishwa kazi wakitarajiwa kurejea kazini.


Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gelard Mweli, wakati akizungumza kuhusu mgogoro uliotokea katika kiwanda hicho baada ya kufungwa kwa takribani miezi mitano, hali iliyosababisha wafanyakazi 216 kusitishiwa ajira na kuandamana wakidai stahiki zao.


Mweli amesema kuwa changamoto kuu tatu zilizoikumba kiwanda hicho zimejadiliwa kwa kina na wadau wote wakiwemo wawakilishi wa wafanyakazi, chama cha wafanyakazi, na serikali, ambapo makubaliano muhimu yamefikiwa ili kuhakikisha uzalishaji unaanza upya kwa wakati.


“Tumejadili kwa uwazi, na tumekubaliana kwamba ndani ya miezi mitatu kiwanda kianze kufanya kazi ili wakulima waweze kuendelea na uuzaji wa chai yao kama kawaida. Wafanyakazi nao watarudi kazini mara tu taratibu za malipo yao zitakapokamilika,” amesema Mweli.



Amefafanua kuwa kusitishwa kwa ajira hakukutokana na makosa ya wafanyakazi, bali kutokana na changamoto za kifedha zilizomkumba mwekezaji baada ya kiwanda kusimama kwa miezi kadhaa bila uzalishaji. Hata hivyo, serikali imeahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa.


“Serikali ipo bega kwa bega na wakulima na wafanyakazi. Hakuna haki ya mfanyakazi itakayopotea. Tumekubaliana na chama cha wafanyakazi kuhakikisha haki zote zinalindwa na kila upande unatekeleza wajibu wake ipasavyo,” aliongeza Mweli.


Aidha, amewatoa hofu wakulima wa chai wa Rungwe akisema serikali inaendelea kufanya kazi kwa karibu na mwekezaji kuhakikisha kiwanda kinaanza uzalishaji mapema ili sekta ya chai iendelee kuchangia katika uchumi wa wananchi wa eneo hilo.




🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE CHANNEL Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post