Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Serikali imewataka wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na serikali katika juhudi za kuongeza ujuzi kwa wakulima na wazalishaji wadogo ili kupanua wigo wa manufaa ya sekta ya kilimo nchini.
Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bi. Zuhura Yunus, wakati akifungua Mafunzo ya Kuongeza Ujuzi kwa Wakulima na Wasindikaji Wadogo katika Sekta ya Kilimo.
Bi. Zuhura alisema serikali inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wakulima wanapata ujuzi unaowawezesha kuongeza tija na thamani ya mazao yao, sambamba na kukuza kipato na kuchangia katika pato la taifa.
“Natoa wito kwa wadau wote waendelee kuunga mkono jitihada hizi. Ujuzi ni mtaji na kichocheo cha maendeleo. Tunataka kuona wakulima wakitumia fursa hii kujifunza kwa bidii na kuwa mabalozi wa mabadiliko katika maeneo yao,” amesema Bi. Zuhura.
Ameongeza kuwa serikali inalenga kuhakikisha mchango wa sekta ya kilimo katika pato la taifa unaongezeka kutoka asilimia 4.6 mwaka 2025 hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, kupitia mikakati ya kujitosheleza kwa chakula, kuongeza kipato cha wakulima, na kuchochea ukuaji wa viwanda.
Kwa mujibu wa Bi. Zuhura, kilimo kinaendelea kuwa mhimili wa uchumi wa taifa, kikichangia asilimia 26.5 ya Pato la Taifa, kuajiri asilimia 65 ya nguvu kazi, na kuchangia asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje.
Aidha, amesema serikali imeanzisha mfuko wa dhamana kupitia Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na Benki ya Ushirika ili kuwawezesha wakulima na wazalishaji wadogo kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.
“Tunataka wakulima wawe na mtaji wa kutosha, ujuzi wa kisasa na miundombinu bora ya kuongeza thamani ya mazao yao. Haya ndiyo mageuzi tunayoyalenga katika sekta hii,” aliongeza Bi. Zuhura.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dkt. Thomas Bwana, alisema taasisi yake imepiga hatua kubwa katika utafiti na ubunifu wa teknolojia zinazolenga kuboresha kilimo nchini.
“Katika miaka ya karibuni tumewekeza sana katika tafiti, miundombinu ya maabara na umwagiliaji,”
Tumeboresha uwezo wa watafiti wetu kupitia masomo, mafunzo na teknolojia mpya. Haya yote yanalenga kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora na teknolojia zinazokabiliana na changamoto za kilimo,” amesema Dkt. Bwana.
Aliongeza kuwa TARI ina majukumu makuu matatu, likiwemo kufanya tafiti za kisayansi kutatua changamoto za wakulima, kuzalisha mbegu bora, na kukuza teknolojia za kuongeza tija katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo.
“Tunafanya kazi kuanzia katika udongo hadi mavuno — kuhakikisha kila mkulima ana maarifa sahihi ya matumizi ya udongo, mbegu bora na teknolojia za umwagiliaji,” alifafanua Dkt. Bwana.
Mafunzo hayo yamejikita zaidi katika vitendo ili kuwawezesha wakulima kuona kwa macho na kushiriki moja kwa moja katika mafunzo, jambo linalotarajiwa kuongeza uelewa na kuleta mabadiliko chanya katika kilimo cha kisasa chenye tija.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.






