Dodoma.📍
Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, ameendelea na kampeni zake katika Kata ya Mtumba ambapo amewaomba wananchi kumpa ridhaa ya kuwa mbunge wa kwanza wa jimbo hilo jipya, akiahidi kuwaletea maendeleo makubwa kwenye sekta mbalimbali.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika kata hiyo, Mavunde amesema endapo ataaminiwa na wananchi katika uchaguzi mkuu ujao, ataanza kwa kuboresha miundombinu ya elimu, ikiwemo ujenzi wa Shule ya Sekondari Vikonje A na Shule ya Msingi Vikonje B.
Amesema atahakikisha anasimamia na kuvutumia ujenzi wa shule za Sekondari na Msingi kwa kushirikisha Taasisi binafsi na za umma ili kuchochea maendeleo ya sekta ya elimu ndani ya Kata ya Mtumba.
Aidha, Mavunde amebainisha kuwa kuanzia mwezi Novemba mwaka huu, atanunua mitambo 20 ya kudurufu mitihani ili kupunguza mzigo kwa wazazi wanaolazimika kuchangia gharama za mitihani kila mara.
Amesema mashine hizo zitasambazwa katika kila kata ya Jimbo la Mtumba ili kuwezesha shule zote kutoa mitihani bila usumbufu.
Katika hatua nyingine, Mavunde amegusia kundi la wazee akisema limesahaulika kwa muda mrefu, na kwamba atahakikisha anaunda klabu za wazee zitakazokuwa jukwaa la kusikiliza changamoto zao,
Pia, ataanzisha Anthony Mavunde Foundation, taasisi itakayolenga kusaidia makundi yasiyojiweza katika jamii.
Akihitimisha hotuba yake, Mavunde amesema serikali tayari imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa umeme unaotarajiwa kunufaisha maeneo yote ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo.
Amesema kata ya Mtumba ni miongoni mwa maeneo yatakayopata manufaa ya moja kwa moja, huku akiwataka wananchi wa Mtumba kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kumpa kura ili aweze kutimiza ahadi hizo za maendeleo kwa vitendo.
🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.








