Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, ameahidi kusimamia ukamilishaji wa mradi wa upimaji na umilikishaji wa ardhi kwa wananchi wa Kata ya Chahwa, ikiwa ni sehemu ya mikakati yake ya kutatua changamoto zinazowakabili wakazi wa eneo hilo.
Katika mwendelezo wa kampeni zake, Mavunde amebainisha kuwa changamoto ya ardhi imekuwa kero kwa wananchi wengi wa Chahwa, hivyo ameweka kipaumbele kuhakikisha wananchi wote wanaonyeshwa maeneo yao na kumilikishwa rasmi.
Ameeleza kuwa atahakikisha ofisi ya ardhi ya Jiji inaweka kambi katika Kata ya Chahwa ili huduma ziwe karibu zaidi na wananchi.
Pia amezungumzia changamoto ya maji katika mitaa ya Muongozo na Muungano, akisema kuwa mradi wa maji umefikia asilimia 75 na kwamba atahakikisha asilimia 25 zilizobaki zinakamilishwa mapema ili wananchi wote wapate huduma ya maji safi na salama.
Kupitia kampeni zake, Mavunde amesisitiza umuhimu wa kuchimba visima vya maji kwa ajili ya shughuli za kilimo cha umwagiliaji, akilenga kuwawezesha vijana kunufaika na fursa za uzalishaji kupitia kilimo.
Aidha, amesema kuwa mpango wa Serikali kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwawezesha vijana kupitia kilimo cha umwagiliaji, ambapo Serikali imepanga kuchimba visima elfu 68 nchini kote, na Kata ya Chahwa ni miongoni mwa maeneo yatakayofaidika na mpango huo.
🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.





