Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mgombea wa udiwani kata ya Uhuru, Hassan Makamba, ameahidi mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii endapo atachaguliwa katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata ya Uhuru, Makamba alisema kipaumbele cha kwanza kitakuwa mikopo ya asilimia 10 kwa walemavu, vijana na wazee, pamoja na kuanzisha programu mbalimbali za ujasiriamali.
Alibainisha kuwa kata ya Uhuru imejaa wafanyabiashara na wajasiriamali, hivyo suluhisho la kukuza uchumi ni kuwawezesha wananchi kuelewa njia bora za kukusanya mitaji, kupata mikopo na kuendesha shughuli za biashara kwa mafanikio.
“Kama mfanyabiashara ambaye nimeishi changamoto za kata hii kwa muda mrefu, nazifahamu matatizo yote yanayowakabili wananchi,” alisema Makamba.
“Wananchi wana imani kubwa nami kwa sababu nimekuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku, na changamoto walizo nazo ndizo ambazo nami nimezipitia. Nikipewa ridhaa nitazitatua ndani ya baraza.”
Makamba aliwapongeza wenzake wa CCM waliogombea nafasi hiyo lakini hawakuteuliwa, akisisitiza kuwa hakuna aliyeshindwa bali mchakato umefuata taratibu za chama.
“CCM hakuna anayeshindwa, ni mchakato. Wale ambao hawakuteuliwa bado ni sehemu ya familia yetu na ipo siku watapata nafasi,” alisema.
Alimalizia kwa kuwataka wananchi kumpa ridhaa sambamba na kumpigia kura Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mbunge Pascal Chinyele, akiahidi maendeleo ya hali ya juu kupitia mshikamano na mshirikiano wa pamoja.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.







