MKUU WA MKOA WA DODOMA AWATAKA WANAUSHIRIKA KUTUMIA MIUNDOMBINU YA KISASA KUCHOCHEA UCHUMI

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amewataka wanaushirika wa mkoa huo kutumia kikamilifu fursa za miundombinu ya kisasa iliyowekwa na serikali, ikiwemo uwanja wa ndege wa kisasa, reli ya kisasa ya SGR na barabara ya mzunguko, ili kuongeza tija katika kusafirisha mazao na kukuza uchumi wa wanachama.


Akizungumza leo tarehe 19 Septemba 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma wakati wa usajili wa washiriki wa kikao cha wadau wa ushirika, Senyamule amesema miradi hiyo mikubwa haipaswi kushangiliwa tu bali itumike kama chachu ya maendeleo ya kiuchumi.


“Kila fursa mnayoisikia mnatakiwa muitafsiri kama manufaa ya kiuchumi. Dodoma ndiyo mkoa pekee ulionufaika zaidi na miradi hii ya kimkakati. Hii si bahati mbaya, bali ni matokeo ya juhudi za serikali yetu kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema.


Senyamule amebainisha kuwa utaratibu wake wa kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii ni sehemu ya kukuza uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi. 


Alisema vikao kama hivyo vina lengo la kutoa mrejesho kuhusu mafanikio ya serikali, kupokea maoni ya wananchi, na kusikiliza changamoto zinazokabili vyama vya ushirika.


Almeongeza kuwa sekta ya ushirika ni nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania na kwamba vyama vingi vya ushirika vimeanza kuimarika kutokana na sera na taratibu mpya zilizowekwa na serikali.


“Nashukuru serikali yetu kupitia Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameimarisha taratibu na sheria za vyama vya ushirika, jambo ambalo limewezesha sekta hii kuendelea kustawi,” alisisitiza.


Aidha, amewataka wanaushirika kutambua mchango wa miradi ya kimkakati katika kuongeza mapato, kupunguza gharama za uzalishaji, na kupanua masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi.


Kikao hicho kiliwaleta pamoja viongozi wa vyama vya ushirika, wadau wa maendeleo, na maafisa wa serikali, kikilenga kujadili mbinu za kuboresha sekta hiyo katika mkoa wa Dodoma.







🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post