DKT. SANGA: TUKISHIKAMANA TUTASHINDA KWA KISHINDO

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.

Dkt. Tumaini Sanga leo Septemba 5, 2025 ameongoza uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Chang’ombe, jijini Dodoma, kwa ajili ya kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Dodoma Mjini, Mhe. Paschal Chinyele.


Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyohudhuriwa na wanachama na wapenzi wa CCM, Dkt. Sanga alisema uzinduzi huo ni mwanzo wa harakati rasmi za kuhakikisha chama kinashinda kwa kishindo ifikapo Septemba 29, siku ya kupiga kura.


Alikiri kuwa miongoni mwa waliochukua fomu kuomba ridhaa ya CCM kugombea ubunge katika jimbo hilo, lakini hakubahatika kupitishwa. Hata hivyo, alisisitiza kuwa kutopitishwa hakumaanishi mwisho wa safari ya kisiasa bali ni nafasi ya kumuunga mkono aliyeteuliwa na chama.


“Cha kwanza ni kumuunga mkono mgombea ambaye ameweza kushika nafasi hii na kukubalika na chama. 

Hatuna budi kushirikiana kumpigania kura zote ili ashinde kwa kishindo,” alisema Dkt. Sanga huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano ndani ya chama.


Aliongeza kuwa yeye binafsi hakuendelea na makundi baada ya jina lake kutojitokeza, bali alirejea kushughulikia majukumu ya chama katika kata yake na sasa yupo bega kwa bega na mgombea wa chama hicho.



Akizungumzia nafasi ya wanawake katika uongozi wa kitaifa na kisiasa, Dkt. Sanga alisema mafanikio ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yamekuwa chachu kubwa ya kuwainua wanawake wengi kujiamini na kushiriki kwenye nafasi mbalimbali za uongozi.


“Wanawake na vijana wanajifunza zaidi kwa kutazama mfano wa mbele. Rais Samia ni mfano halisi wa ujasiri na uthubutu. Ameonyesha kuwa hakuna nafasi inayoshindikana kwa mwanamke iwe kata, wilaya, jimbo, taifa au hata katika nyanja nyingine za kitaaluma na biashara,” alieleza.


Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi wa CCM wa kata, wilaya na mkoa, pamoja na makundi ya wanachama waliokubaliana kuhakikisha Mhe. Paschal Chinyele anapigiwa kura za ndiyo katika uchaguzi ujao.







🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post