TATA INTERNATIONAL YAWAKUMBUKA WAKULIMA, YAWAPA TEKNOLOJIA NA OFA KABAMBE NANENANE

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Wakulima na wafugaji nchini wametakiwa kuachana na mazoea ya kizamani na badala yake kujikita katika matumizi ya teknolojia bora na za kisasa ili kuongeza kasi ya uzalishaji, kukuza kipato na kuchangia katika pato la Taifa.


Wito huo umetolewa jijini Dodoma katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni, ambapo washiriki mbalimbali kutoka sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi wamehimizwa kutumia maonesho hayo kama fursa ya kujifunza mbinu mpya na bora za uzalishaji.


Bw. Smart Deus, Meneja Masoko na Mauzo wa Tata International, alisema kampuni yao imejikita katika kusaidia wakulima na wafugaji kupitia mnyororo wa thamani, ikiwemo kuwawezesha katika usafirishaji wa mazao na bidhaa kutoka shambani hadi sokoni.


Tumeshiriki Nanenane ili kuwahakikishia wakulima urahisi wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Tumewaletea magari ya kubebea mazao na mizigo, ili kumrahisishia mkulima kufikisha bidhaa yake sokoni kwa wakati, alisema Deus.


Aliongeza kuwa msimu huu kampuni hiyo imetoa ofa maalum kwa wakulima, wafugaji na wafanyabiashara, na kuwakaribisha wananchi kutembelea banda lao lililopo mkabala na Benki Kuu kwenye viwanja vya maonesho.



Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa Tata International, Bw. Elia Rajabu, alisema kampuni hiyo imejikita kutoa suluhisho bora kwa wakulima kupitia mauzo ya trekta za kisasa za John Deere ambazo zina ubora wa kimataifa na zinatoa matokeo ya haraka shambani.


Katika Nanenane tumekuja na ofa za kipekee kwenye trekta na spea zake. Wateja watakaonunua bidhaa zetu wanapata punguzo maalum, pamoja na dhamana ya miaka miwili au masaa 2,000 ya matumizi, alisema Rajabu.


Maonesho ya Nanenane kwa mwaka 2025 yamebeba kaulimbiu: “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”, na yamevutia washiriki kutoka sekta mbalimbali ikiwemo taasisi za kifedha, vyuo vya utafiti, mashirika ya umma na binafsi, pamoja na wajasiriamali wa kilimo.


Kwa mujibu wa waandaaji, maonesho hayo yanaendelea kwa mafanikio makubwa huku teknolojia mpya na suluhisho bunifu zikionesha jinsi zinavyoweza kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo na mifugo nchini.








🚨Full Video inapatikana katika YOUTUBE CHANNEL Yetu ya WASHINDI MEDIA

Previous Post Next Post