SERIKALI YAZINDUA UJENZI WA MAABARA YA KISASA YA MADINI – WACHIMBAJI KUNUFAIKA

 


Na Carlos Claudio,Dodoma.


Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema serikali imejipanga kuhakikisha wachimbaji wa madini nchini wanapata msaada wa kitaalamu kupitia huduma za maabara ya kisasa inayojengwa jijini Dodoma, chini ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).


Akizungumza leo wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa maabara hiyo, Mhe. Mavunde amesema serikali inalenga kuwasaidia wachimbaji kuachana na uchimbaji wa kubahatisha, na badala yake watumie taarifa sahihi za kisayansi ili kupunguza gharama na kuongeza tija.


Maabara hii ni mkombozi mkubwa kwa wachimbaji wa Tanzania. Itawawezesha kupata matokeo ya uhakika, kwa haraka na kwa gharama nafuu, jambo litakalowasaidia kuongeza ufanisi na kuchochea ukuaji wa sekta ya madini nchini,amesema Mhe. Mavunde.


Ameeleza kuwa bajeti ya Wizara ya Madini imeelekezwa zaidi katika uwekezaji wa utafiti, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiridhia mchakato wa ununuzi wa helikopta kwa ajili ya kufanya utafiti wa awali (geophysical survey). 



Aidha, miradi mikubwa ya kurusha ndege kufanya utafiti katika vitalu sita inatarajiwa kuanza hivi karibuni, ikihusisha eneo la zaidi ya kilomita za mraba 164,774, sawa na asilimia 18 ya eneo lote la Tanzania.


Hatuwezi kukuza sekta ya madini bila kuwekeza katika utafiti. Ndiyo maana tumeamua kujenga maabara hii kubwa na ya kisasa, ambayo si tu itahudumia Tanzania, bali pia nchi jirani za Afrika Mashariki na Kati,”amesema Waziri Mavunde.


Kwa mujibu wake, serikali inalenga kuhakikisha wachimbaji wanapata taarifa sahihi na kwa wakati, huku ikiwajengea uwezo wataalamu wa GST kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali ikiwemo kampuni ya GTK.


Maabara hiyo ikikamilika, inatarajiwa kuwa moja ya kubwa zaidi katika kanda ya Afrika Mashariki na Kati, hatua itakayoweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa katika utafiti na uchambuzi wa madini.







🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post