Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mgombea wa nafasi ya Udiwani Kata ya Mkonze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Robert Jonas Njama, ameahidi kuwa mwadilifu na kushirikiana kwa karibu na wananchi pamoja na viongozi wa chama na serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa kata hiyo.
Akizungumza na Washindi Media jijini Dodoma mara baada ya kuchukua fomu ya udiwani ya kuwatumikia wananchi wa kata ya Mkonze kupitia Chama Cha Mapunduzi, Njama alisema uteuzi wake ni heshima kubwa na deni kwa wananchi wa Mkonze waliompa imani ya kupeperusha bendera ya CCM.
“Nichukue nafasi hii kuwashukuru wananchi wa Mkonze na wajumbe wote wa CCM kwa kunipendekeza kuwa diwani wao. Nitaendelea kushirikiana na viongozi wa chama, serikali za mitaa na wananchi kuhakikisha changamoto mbalimbali tunazimaliza kwa pamoja,” alisema Njama.
Aidha, alisisitiza kuwa hakuna kiongozi anayeweza kuingia madarakani na kumaliza changamoto zote, bali jukumu la msingi ni kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na kuendeleza miradi iliyopo.
“Nitahakikisha ninaanzia pale alipoishia kiongozi aliyekuwa madarakani, lakini pia nitashirikiana naye kuhakikisha miradi inakamilika sambamba na kuibua miradi mipya kwa ajili ya vijana,” aliongeza.
Njama pia aliwashukuru wananchi na makundi mbalimbali ikiwemo waendesha bodaboda kwa kujitokeza kwa wingi kumuunga mkono, akibainisha kuwa mshikamano huo unaonesha imani kubwa aliyopewa na jamii.
Kwa upande wake, Gakala Lububu, mkazi wa Mkonze, alisema uteuzi wa Njama unadhihirisha imani ya chama na wananchi kwa mgombea huyo miongoni mwa wagombea 18 waliokuwa wamejitokeza kuchukua fomu.
“Nilimpongeza kwa sababu ni mtu niliyemwamini na naamini atapeperusha bendera ya chama kwa heshima. Chama kipo sehemu salama kupitia yeye,” alisema Lububu.
Wananchi wa Mkonze wameendelea kuonesha mshikamano na matumaini makubwa kuwa mgombea huyo ataibua miradi mipya na kusimamia sekta muhimu ikiwemo afya, maji, ardhi na miundombinu ili kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanapatikana.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.