Na Carlos Claudio, Dodoma.
Wakazi wa Mtanana jijini Dodoma sasa wanapumua kwa furaha baada ya Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kukamilisha ujenzi wa tuta la barabara lenye urefu wa kilometa sita, hatua iliyotatua kabisa kero ya mafuriko yaliyokuwa yakijitokeza mara kwa mara hasa wakati wa mvua kubwa za El-Nino.
Akizungumza jana jijini Dodoma, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, alisema eneo la Mtanana lilikuwa kero kubwa kila msimu wa mvua kutokana na maji mengi kutoka milimani kuzidi makalavati na daraja lililokuwepo, hali iliyosababisha mafuriko na kuwazuia wananchi kutumia barabara kwa saa kadhaa.
“Mbali na kunyanyua tuta hili, tumejenga makalavati makubwa saba yenye uwezo mkubwa wa kupitisha maji kwa wakati mmoja. Hii ni tofauti na awali ambapo makalavati yaliyokuwepo yalizidiwa na maji mengi na hivyo kusababisha barabara kufungwa kwa muda mrefu,” alisema Mhandisi Zuhura.
Aliongeza kuwa mradi huo unaosimamiwa na TANROADS mkoa wa Dodoma na kutekelezwa na kampuni ya kitanzania ya Estim Construction ulianza Juni 13, 2024 na ulitarajiwa kukamilika Novemba 13, 2025, lakini hadi sasa umeshakamilika kwa asilimia 97.
“Mkandarasi amefanya kazi kwa bidii ikiwemo kufanya kazi zaidi ya muda, na ameshakamilisha ujenzi wa madaraja, kuinua tuta, kuweka kifusi na lami. Kilichobaki ni uwekaji wa alama za barabarani na taa za usalama,” alisema.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa mkandarasi Estim Construction, Mhandisi Mussa Mwaipopo, aliishukuru serikali na TANROADS kwa ushirikiano walioupata kipindi chote cha ujenzi. “Hatukukumbana na changamoto yoyote kubwa. Serikali imekuwa ikitulipa kwa wakati na muda si mrefu barabara hii itakabidhiwa rasmi kwa matumizi,” alisema.
Naye mkazi wa Mtanana na Afisa Usafirishaji, Pascal Robert, alitoa ushuhuda wa namna wananchi walivyotaabika kabla ya mradi huo kutekelezwa. “Hapa magari yalilazimika kuegeshwa pembeni kwa zaidi ya saa 20 yakisubiri maji yapungue. Hata sisi waendesha bodaboda tulikuwa hatuwezi kupita. Tunashukuru serikali kwa utekelezaji wa ahadi yao, lakini tunaiomba pia wakamilishe uwekaji wa taa ili kuimarisha usalama hususan nyakati za usiku,” alisema.
Mradi huu wa thamani ya Shilingi Bilioni 26.15 ni sehemu ya jitihada za serikali kuboresha miundombinu ya barabara nchini na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za usafirishaji bila vikwazo vya mafuriko.