Na Carlos Claudio, Dodoma.
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema kuwa mfumo wa JamiiStack umeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuunganisha mifumo ya kiserikali na ile ya sekta binafsi, hivyo kuchochea maendeleo ya kidijitali nchini Tanzania – hasa kwa wakulima na wadau wengine wa maendeleo walioko maeneo ya vijijini.
Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima Nanenane yanayoendelea kwenye Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Afisa TEHAMA wa Wizara hiyo, Kiswigu Mwakisisya, alifafanua kuwa JamiiStack ni mfumo jumuishi unaowezesha mifumo mbalimbali ya kidijitali kusomana, kubadilishana taarifa kwa usalama na kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa kwa wananchi wote.
Mwakisisya ameeleza kuwa JamiiStack ni mkusanyiko wa teknolojia muhimu za msingi – zinazojulikana kama Digwital Public Infrastructure (DPI) – ambazo zimeundwa kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa njia ya kidijitali. Mfumo huu umejengwa kwa kuzingatia viwango vya juu vya usalama, faragha na haki za mtumiaji wa mwisho.
Mfumo wa JamiiStack una sehemu kuu tatu:
1. Mazingira Wezeshi ya Kiteknolojia
Hii inajumuisha uwepo wa miundombinu muhimu kama vile:
- Minara ya mawasiliano;
- Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaounganisha wilaya zote;
- Nishati ya umeme inayotegemewa na mifumo ya TEHAMA;
- Sera, sheria na miongozo inayosimamia matumizi salama na madhubuti ya TEHAMA nchini.
2. Miundombinu ya Kidijitali ya Umma
Hii sehemu inahusisha mifumo mitatu muhimu:
- Jamii Namba – mfumo wa utambulisho wa kidijitali wa kila raia, kuanzia umri wa miaka 0. Namba hii hufanana na ile ya NIDA, na hutumika kwa huduma mbalimbali kwa njia salama na ya uhakika.
- Jamii Pay – mfumo wa malipo ya kielektroniki unaoratibiwa na Benki Kuu ya Tanzania kupitia Tanzania Instant Payment System (TIPS).
- Mfumo wa JamiiStack – unaowezesha taasisi na mifumo kuwasiliana kwa pamoja kwa urahisi na usalama.
3. Ubadilishanaji wa Taarifa kwa Usalama
Kupitia mfumo wa Jamii X-Change, taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi zinaweza kushirikiana taarifa kwa viwango sanifu vya kitaifa bila kuhatarisha usalama wa watumiaji, hata katika taarifa zinazovuka mipaka ya nchi.
Afisa huyo alibainisha kuwa mfumo huu una faida kubwa kwa wakulima ikiwa kuwapa taarifa za hali ya hewa, tabia ya udongo na magonjwa ya mazao huku taarifa zikipatikana kupitia simu janja, mitandao au redio jumuishi ambazo hufikia vijijini.
Mwakisisya alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele kikubwa katika kukuza mazingira ya TEHAMA.
Ujenzi wa miundombinu mikubwa kama Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere umesaidia kuongeza nishati ya umeme ambayo ni muhimu katika uendelezaji wa huduma za kidijitali nchini.
Kwa ujumla, mfumo wa JamiiStack umewekwa kama msingi imara wa mageuzi ya kiuchumi na kijamii kupitia teknolojia, ukiunganisha sekta ya umma na binafsi. Mfumo huu unaifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika matumizi ya teknolojia kwa maendeleo jumuishi – hasa kwa wakulima na wananchi wa kawaida walioko pembezoni mwa mifumo rasmi ya huduma.
🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu ya WASHINDI MEDIA