Na Carlos Claudio, Dodoma.
Katika kuunga mkono juhudi za kuinua kilimo kupitia teknolojia, kijana mjasiriamali kutoka mkoa wa Arusha, Rahmani Mbahe, amezindua mfumo wa kisasa unaoitwa Agrocare AI, unaolenga kuwasaidia wakulima kupata taarifa sahihi za shamba lao na kupanga mazao kwa wakati unaofaa.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, ndani ya banda la Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mbahe amesema mfumo huo umetengenezwa kwa kutumia akili Unde (AI), AOT device na teknolojia ya Arduino, unaoweza kugundua hali ya udongo na mazingira ya shamba.
“Kupitia sensa zilizowekwa shambani, mkulima anaweza kupata taarifa za joto la udongo, unyevu (humidity), kiwango cha pH na hali ya hewa moja kwa moja kwenye simu yake janja,” amesema Mbahe.
“Taarifa hizi huchambuliwa na AI ili kumpa mkulima mwongozo wa hatua sahihi za kuchukua kulingana na hali ya shamba.”
Mbali na hilo, mfumo huu una kipengele cha kupiga na kupakia picha za mimea ambapo mkulima hupata utambuzi wa magonjwa na ushauri wa namna ya kuyakabili. “Mkulima ataelezwa tatizo la mmea, chanzo chake na hatua za matibabu,” aliongeza.
Rahmani Mbahe amesema lengo ni kumsaidia mkulima asiye na utaalamu mkubwa wa kilimo kufanya maamuzi kwa kutumia taarifa za kisayansi, hivyo kuongeza tija na kupunguza hasara.
🚨Subscribe YOUTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA