Na Hellen M. Minja, DODOMA.
Serikali inatamani kuwa na vijana wanaojitambua, wenye dira, malengo na ndoto za maisha yao pia wenye kufanya bidii katika kuyafikia malengo hayo. Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule alipohudhuria hafla ya uzinduzi wa mafunzo ya ufundi stadi na ugawaji wa vifaa iliyofanyika kwenye ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Chamwino Jijini Dodoma Julai 08, 2025.
Mhe. Senyamule ameyasema hayo kwa vijana wanaokwenda kuanza mafunzo ya ufundi stadi katika fani mbalimbali chini ya udhamini wa ‘World Vision Tanzania’ na Taasisi ya ‘Tanzania Home Economics Association’ (TAHEA) ambazo kwa pamoja zinatekeleza Mradi wa Vijana Balehe unaolenga kuongeza utambuzi wa masuala ya Afya ya uzazi kwa vijana balehe wa Kike na Kiume (AHADI)
“Tunatamani kama Serikali tuwe na vijana wanaojitambua ambao wana dira, ndoto za maisha yao, malengo, lakini wanafanya bidii kuyafikia hayo malengo. Nyinyi mmepata bahati ya kusikia na kuambiwa kwa hiyo bahati hiyo muitumie, hiyo elimu huko zamani haikuwepo, watu walikua wanakwenda kama vipofu nyinyi mnakwenda kama werevu na wenye maarifa, tumieni vizuri elimu zote ambazo mmepewa”. Mhe. Senyamule.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa TAHEA Bi. Lediana Mng’ong’o amesema wamekabidhi zawadi kwa vijana wawili waliohitimu mafunzo ya ufundi stadi kwa upande wa Upishi ambaye amepewa vitendea kazi vyenye thamani ya shilingi 2,000,000 na aliyehitimu kwa upande wa urembo ambaye nae amepatiwa vifaa vyenye thamani ya shilingi 2,000,000 ili wakatimize ndoto zao.
Aidha, Mhamasishaji wa vijana walio kwenye mradi huo Bi. Scholastika Senga, amesema Vijana waliopewa zawadi kwenye hafla hiyo walionesha moyo wa kujituma kuanzia mwanzo wa mradi hadi mwisho hivyo wamepatiwa zawadi ili kutoa motisha kwa vijana wengine wanaoingia kwenye mafunzo stadi chini ya mradi huo.
Mradi wa AHADI unatekelezwa kwenye majiji ya Dar es salaam na Dodoma kuanzia Aprili 2024 hadi March 2029 ukilenga kuongeza utambuzi wa masuala ya afya ya uzazi na kuwawezesha kiuchumi Vijana Balehe wenye umri wa maika 10-24.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.