Na Meleka Kulwa, Dodoma.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, viongozi wa dini wameendelea kutoa wito wa kudumisha amani nchini, wakisisitiza umuhimu wa maadili, mshikamano na kauli njema katika kipindi hiki.
Akizungumza jijini Dodoma Mchungaji Meshack Tulana Nhuti , anayehudumu katika Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Central Tanganyika, Parishi ya Nhalawanda Nzuguni B Kanisa la St .John Dodoma, amesema kuwa kanisa lina jukumu kubwa katika kuhubiri na kudumisha amani.
Sisi kama kanisa tunahubiri amani. Pale tunapokosa kuhubiri amani, machafuko yanaweza kuingia. Kwa hiyo, tuhubiri amani katika kila hatua, kwa kila mtu.
Amesisitiza kuwa kila kiongozi wa dini anapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kulinda amani ya taifa.
“Sote ni wahubiri wa amani, iwe ni kanisa Katoliki, Anglikana au makanisa ya Kipentekoste. Tunapaswa kuhubiri maneno yanayojenga na sio kubomoa,” amesema
Aidha Mchungaji Meshack akizungumza kuhusu nafasi ya kanisa katika kulinda amani, amesema kuwa taasisi za kidini ni sauti kuu ndani ya jamii, hivyo kiongozi akisema jambo, watu wengi humsikiliza.
“Ukihubiri chuki, watu watafuata chuki, ukihubiri amani, watu wataenenda kwa amani. Tunapaswa kuwa na maadili, utu na kumcha Mungu,” amesisitiza.
Katika kuelekea uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais, Mchungaji Meshack ametoa wito kwa watanzania wote waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga kura kujitokeza kwa wingi na kutimiza haki yao ya msingi ya kupiga kura na kuchagua kiongozi anayefaa.
“Kura ni haki yako ya msingi. Tumia kura yako kuwachagua viongozi unaowaamini. Na wale walioamua kugombea, tunawaombea na kuwasihi kutumia lugha nzuri katika kampeni. Lugha ya matusi au kashfa haitujengi, bali inabomoa taifa,” amesema
Sambamba na hayo amewahimiza vijana na kuwasihi kutumia nafasi zao kikamilifu katika kujenga taifa na kanisa kwa kuwa kizazi hicho ni tegemezi katika ujenzi wa taifa.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.