USHIRIKA WAZIDI KUIINUA TANZANIA, MAUZO YA NJE YAPAA KWA DOLA MILIONI 344


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amewapongeza wakulima wa Tanzania kwa kazi kubwa ya kuzalisha mazao kwa wingi, hatua iliyochochea usalama wa chakula nchini na kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa.


Akizungumza jijini Dodoma Julai 5, 2025, wakati wa kufunga Kongamano la Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani, Dkt. Biteko alisisitiza kuwa sekta ya kilimo kwa sasa inachangia asilimia 26 ya Pato la Taifa (GDP), hali inayodhihirisha nguvu ya wakulima na Vyama vya Ushirika katika uchumi wa taifa.


"Leo hii nchi yetu ina chakula cha kutosha mitaani, si kwa bahati, bali ni juhudi za wakulima na uwezeshaji wa Serikali kupitia vyama vya ushirika," alisema Dkt. Biteko.


Kwa mujibu wa takwimu alizotoa, mwaka wa fedha 2024/25 vyama 1,084 vya ushirika viliuza kahawa na tumbaku moja kwa moja nje ya nchi na kuingiza kiasi cha Dola za Marekani 344.8 milioni, ikilinganishwa na Dola milioni 325.5 zilizopatikana mwaka 2023/24 — ongezeko la Dola milioni 19.3.


Katika hatua ya kuimarisha uwajibikaji, Dkt. Biteko alibainisha kuwa vyama vilivyopata Hati Safi ya Ukaguzi kutoka Shirika la COASCO vimeongezeka kutoka 339 mwaka 2021/22 hadi 631 mwaka 2023/24 — ongezeko la asilimia 86.13. Aidha, vyama vilivyopata Hati isiyoridhisha vimepungua kwa asilimia 78 kutoka 1,198 hadi 263 katika kipindi hicho hicho.


Ametoa rai kwa vyama hivyo kuwawezesha wanawake zaidi na kuongeza idadi ya vyama vya wanawake kutoka 50 vilivyopo sasa.


Licha ya mafanikio hayo, Dkt. Biteko amezitaka Wizara za Fedha na Kilimo kushughulikia kwa haraka changamoto zinazowakabili wakulima, hasa suala la bei ya mazao, pembejeo na huduma muhimu.


“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia inatambua kuwa ushirika ni silaha ya maendeleo ya wananchi, tutaendelea kuusukuma mbele,” alisisitiza.


Akimpongeza Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, Dkt. Biteko alisema kuwa juhudi zake zimelenga kutimiza maono ya Rais Samia ya kumuinua mkulima kiuchumi. Vilevile, alimpongeza Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, kwa maboresho ya kiutendaji, ikiwemo wito wa vyama hivyo kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao kuongeza thamani na masoko.



Kwa upande wake, Mhe. Hussein Bashe alitaja mafanikio ya Serikali katika kuboresha kilimo, ikiwemo kuongeza bajeti, kuanzisha taasisi kama COPRA na kutoa ruzuku kwa wakulima. Pia alizungumzia utekelezaji wa miradi ya umeme na barabara vijijini kuwa kichocheo cha shughuli za kilimo na uchakataji.


“Sasa mkulima anaweza kuanzisha mashine za kuchakata alizeti kijijini kwake kwa sababu kuna umeme na barabara ya uhakika ya kusafirisha bidhaa,” alisema Bashe.


Hata hivyo, alieleza wasiwasi wake kuhusu mzigo mkubwa wa riba kwa wakulima wa tumbaku, ambapo baadhi ya wakopaji hulipa hadi asilimia 15, hali inayopunguza faida na kuathiri ustawi wa kilimo hicho.


“Mfumo wa fedha lazima ubadilishwe ili mkulima apate nafuu. Sasa hivi wakulima wa tumbaku wanalipa riba kubwa kuliko hata wanunuzi,” alisema.


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, alieleza kuwa mkoa huo una vyama vya ushirika 244 na wananchi wanaelewa thamani ya kushirikiana kupitia vyama hivyo.


Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Ndiege, alieleza mafanikio ya kuanzishwa kwa Benki za Ushirika katika mikoa minne na kuimarika kwa usimamizi wa vyama hivyo. Alisisitiza kuwa ushirika si historia bali ni chombo cha mabadiliko ya kiuchumi.


Naye, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC), Bw. Tito Haule, alisema mwaka huu maadhimisho ya 102 yanafanyika kwa mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na ongezeko la wanachama kutoka milioni 6.9 hadi milioni 10. Pia alieleza mchango wa vyama hivyo katika ajira kwa vijana na pato la Serikali kutoka shilingi bilioni 9.5 hadi bilioni 12.5 ndani ya miaka mitatu.


Ameishukuru Serikali kwa kuongeza mtaji wa bilioni 5 katika Benki ya Ushirika na kuimarisha matumizi ya TEHAMA ndani ya vyama.







🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post