Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mamlaka ya Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma imetoa onyo kali kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri vinavyokiuka sheria kwa kuingiza magari mabovu barabarani, ikisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa mara moja kwa wote wanaohusika.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma (RTO), Yusuf Kamota, katika kituo kikuu cha mabasi cha Nane Nane, wakati wa oparesheni endelevu ya ukaguzi wa magari ya abiria.
“Ninatoa wito kwa wamiliki wa vyombo watengeneze vyombo vyao. Vyombo vibovu vinavyoingia barabarani tukikibaini na kukikamata, tajiri na dereva watafikishwa mahakamani bila kusita,” amesema Kamota kwa msisitizo.
Kwa mujibu wa RTO huyo, oparesheni hiyo ni sehemu ya mpango kazi wa kudumu wa kuhakikisha usalama wa wasafiri ndani ya Mkoa wa Dodoma, ambapo ukaguzi wa magari unafanyika saa 24 kila siku kupitia kitengo maalum cha ukaguzi kilichopo ndani ya stendi hiyo.
“Tunao vehicle inspectors wa kutosha ambao wanakesha hapa. Tunatumia pia mfumo wa kidigitali wa TVS kufuatilia mwendokasi wa magari yote. Kama gari imekiuka kasi inayoruhusiwa, hatua kali huchukuliwa papo hapo,” aliongeza.
Aidha, Kamota amesema doria za usalama barabarani zinafanyika mchana na usiku kupitia highway patrols katika maeneo ya mipaka ya Mkoa wa Dodoma kama Bahi, Kongwa, Mtera, Kondoa na Bareko ili kuhakikisha hakuna gari linalotoroka ukaguzi.
Katika ukaguzi wa leo, jumla ya magari 40 ya abiria yalikaguliwa, ambapo magari matano (5) yalikutwa na mapungufu mbalimbali. Baadhi yatapewa muda kurekebisha dosari hizo huku mengine yakitarajiwa kufungiwa kabisa kwa kuhatarisha maisha ya abiria.
“Hatua zetu ni kali. Tumezungumza na madereva kuhusu wajibu wao, tukatoa elimu kwa abiria ndani ya magari, na sasa muda wa kuchukua hatua umefika. Tutafungia leseni, na kuwapeleka wote wanaokiuka sheria mahakamani,” alisema RTO huyo kwa ukali.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limewahakikishia wakazi wa jiji hilo kuwa litaendelea kuhakikisha kila msafiri anasafiri kwa usalama, uangalizi na kwa kufuata sheria bila shuruti.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.