TRA YAMFIKISHA MAHAKAMANI MFANYABIASHARA STANLEY KWA TUHUMA ZA UKWEPAJI KODI


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Dodoma imemfikisha mahakamani mfanyabiashara Edson Raphael Stanley kwa makosa manane ya kukwepa kulipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), yakiwemo makosa ya uhujumu uchumi, ambayo yamesababisha serikali kupoteza zaidi ya Shilingi milioni 675.


Akizungumza na waandishi wa habari katika viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma leo Julai 18,2025 Meneja Msaidizi wa Huduma kwa Mlipakodi wa TRA mkoa wa Dodoma, Bw. John Njau, amesema kuwa mshtakiwa huyo alikuwa akiwasilisha taarifa za mapato (returns) lakini amekuwa halipi kodi stahiki kwa muda mrefu.


"Malimbikizo ya kodi yamefikia kiasi cha Shilingi milioni 675, hali iliyotulazimu kumfikisha mahakamani. Tunatumia nafasi hii kuwakumbusha wafanyabiashara wote wenye madeni ya kodi, ambayo hayako kwenye mpango maalum wa ulipaji, wajitokeze mara moja TRA kuweka utaratibu wa kulipa kwa awamu," amesema Njau.


Bw. Njau ameongeza kuwa TRA inaendelea kutoa fursa ya makubaliano ya ulipaji wa kodi kwa awamu kwa wale walipakodi wanaoshindwa kulipa kwa wakati mmoja, akisema kuwa utaratibu huo upo kisheria na haufungamanishwi na adhabu ya mara moja.



Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mkuu, Bw. Medalakini Emmanuel, amesema kuwa mshtakiwa amefikishwa mahakamani leo kwa mashtaka 8, ambapo 7 ni ya kushindwa kulipa VAT kati ya Julai 2024 hadi Machi 2025, na kosa la nane ni la uhujumu uchumi kwa kuisababishia serikali hasara kubwa ya mapato.


"Upelelezi wa shauri hili umekamilika, lakini tunasubiri kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili mahakama hii iweze kupewa mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi hii," amesema Emmanuel.


Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma imeahirisha kesi hiyo hadi Agosti 4, 2025, kwa ajili ya hatua zaidi. Kwa mujibu wa sheria, kutokana na kiasi cha fedha kinachohusika kuzidi Shilingi milioni 300, Mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana, hivyo mshtakiwa atalazimika kuwasilisha maombi yake katika Mahakama Kuu.








🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post