![]() |
Na Carlos Claudio, Dodoma.
Katika hatua kubwa ya kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo nchini, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, Julai 16, 2025, amezindua rasmi kampeni ya “Mali Shambani” pamoja na mfumo mpya wa kidijitali wa huduma za ugani uitwao “Ugani Kiganjani”, katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Bashe amesema kuwa mfumo huo unalenga kuwasajili wakulima milioni saba kote nchini, huku akieleza kuwa serikali imejipanga kwa dhati kuwafikia wakulima kwa njia ya kiteknolojia na kuwahudumia kwa ukaribu zaidi.
“Tutawaingiza kwenye mfumo huu maafisa ugani waliothibitishwa na serikali ili kuwaondoa ‘makanjanja’ wasio na sifa. Mkulima atakapojiunga na mfumo, ataweza kuona ni maafisa ugani wangapi wapo katika eneo lake,” amesema Bashe.
Amefafanua kuwa kila afisa ugani anayemhudumia mkulima atawajibika kujaza fomu za utendaji kazi ndani ya mfumo huo, hali itakayoiwezesha serikali kujua ni nani aliyemhudumia mkulima, nani aliyemshauri vibaya, na hata kufuatilia waliosambaza pembejeo feki.
Aidha, amebainisha kuwa kupitia mfumo huu, serikali itakuwa na database ya maafisa kilimo walio nje ya mfumo rasmi wa ajira, ambao wanaweza kusaidia kuziba pengo la upungufu wa wataalam waliopo sasa.
Katika hatua nyingine, Waziri Bashe ametangaza kuwa makao makuu ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) yatahamia rasmi katika kituo kipya cha utoaji wa huduma za kilimo jijini Dodoma, ambacho kitazinduliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Tutakuwa na vituo vitano kama hiki nchini. Kituo hiki kitakuwa na maabara kwa ajili ya kuhudumia wanunuzi wa mazao, hasa kwa ajili ya bidhaa zinazokwenda nje ya mipaka ya Tanzania,” aliongeza.
Vilevile, Bashe alieleza kuwa serikali itawaruhusu Watanzania wenye nembo na bidhaa zao kusaga katika mashine za serikali kwa kuchangia huduma kidogo, jambo litakalowapa wakulima thamani zaidi ya mazao yao.
Waziri Bashe alitumia jukwaa hilo pia kuelezea mafanikio ya awali ya Programu ya BBT (Building a Better Tomorrow), iliyozinduliwa miaka michache iliyopita.
Amesema majaribio ya awali yalifanyika kwa maafisa ugani vijana kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine katika kata 40 nchini, na sasa programu hiyo imepanuka hadi kata 232, jambo ambalo limechochea uzalishaji mkubwa wa pamba ambao unatarajiwa kuvunja rekodi tangu Tanzania ipate uhuru.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kongwa, Mhe. Job Ndugai, amewataka maafisa ugani kutambua kuwa likizo imekwisha rasmi. Ametoa wito kwa ushirikiano wa dhati katika kulinda kituo hicho kipya cha huduma za kilimo, akisisitiza kuwa wizi na udokozi haviwezi kuvumiliwa.
“Tuna fursa mbele yetu, tuitumie kikamilifu kwa maendeleo ya taifa letu. Tusilale!” alihitimisha Ndugai.
Uzinduzi wa mfumo wa Ugani Kiganjani na kituo hiki kipya ni hatua muhimu ya mageuzi makubwa ya kilimo nchini, hasa katika wakati huu ambapo sekta hiyo imebeba matumaini ya ajira, chakula, na uchumi wa viwanda.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.