Na Wellu Mtaki, Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amezitaka taasisi za DUWASA, TANESCO na TANROADS mkoa wa Dodoma kuhakikisha zinashughulikia kwa haraka miundombinu ya maji, umeme na barabara katika jengo la Shirika la Viwango Tanzania (TBS), maarufu kama “Viwango House” linaloendelea kujengwa katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma.
Akizungumza leo wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika eneo la mradi huo, Mhe. Majaliwa amesema kuwa miundombinu bora ni hitaji muhimu kwa jengo hilo ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mara baada ya kukamilika.
“Jengo hili linahitaji miundombinu ya kisasa na bora – maji, umeme na barabara – ili kuhakikisha shughuli zote za TBS zinafanyika kwa ufanisi na kwa viwango vya juu,” amesema Waziri Mkuu.
Aidha, Majaliwa amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya sita inatambua umuhimu wa viwango vya ubora katika maendeleo ya nchi, akieleza kuwa viwango si tu vinaimarisha ubora wa bidhaa, bali pia vinaathiri moja kwa moja afya za wananchi na ukuaji wa uchumi wa taifa.
“Tunahitaji viwanda vyetu vizalishe bidhaa zinazokidhi viwango vya kimataifa, ili ziweze kuuzwa si tu ndani ya nchi, bali hata kwenye masoko ya kimataifa,” ameongeza.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 76 na unatarajiwa kugharimu takribani shilingi bilioni 25.3, gharama inayojumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) pamoja na malipo ya mshauri elekezi. Jengo hilo linatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 30, 2025.
TBS inatarajiwa kutumia jengo hilo kama makao yake makuu mapya, huku likitarajiwa kuwa kitovu cha shughuli za kusimamia viwango vya bidhaa na huduma nchini.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.