Na Carlos Claudio, Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ametoa wito mkali kwa wachimbaji wa madini nchini kuhakikisha wanauza madini yao kupitia masoko rasmi ya serikali ili kuhakikisha rasilimali hizo zinanufaisha taifa.
Akizungumza leo jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa mitambo na vitendea kazi kwa wachimbaji wadogo vilivyotolewa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa uuzaji wa madini nje ya mfumo rasmi ni hasara kwa taifa.
“Natoa wito kwa wachimbaji wote kuuza madini kwenye masoko yetu rasmi (masoko 43) na si kuyatorosha kwenda nchi za nje. Tuwe wazalendo, tutangulize maslahi ya taifa letu,” amesema Majaliwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, akesema kuwa sekta ya madini imepiga hatua kubwa na tayari imevuka malengo ya mwaka 2025 kwa kuchangia asilimia 10.1 ya Pato la Taifa, kabla ya muda wa lengo hilo kufika.
Aidha, alifafanua kuwa mapato kutoka sekta hiyo yameongezeka kwa kasi kutoka shilingi bilioni 162 mwaka 2015/2016 hadi shilingi trilioni 1.04 mwaka 2024/2025, sawa na asilimia 104 ya lengo la makusanyo ya mwaka.
“Marekebisho ya sheria ya mwaka 2017 yalileta mageuzi makubwa. Leo hii, sekta ya madini si tu inachangia pato kubwa kwa taifa, bali imekuwa mfano wa mafanikio ya usimamizi bora wa rasilimali,” amesema Mavunde.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wadau wa sekta ya madini na wachimbaji wadogo kutoka maeneo mbalimbali nchini.
"Kishindo Kingine Cha Awamu ya Sita, Ukombozi kwa Wachimbaji Wadogo Nchini" — Kauli mbiu hii ndiyo iliyoongoza hafla hiyo, ikiakisi dhamira ya serikali katika kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata nguvu mpya ya kiuchumi, kiteknolojia na kisheria ili kushiriki kikamilifu katika mapinduzi ya sekta ya madini.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye Instagram Page yetu ya WASHINDI MEDIA.