DODOMA YANG’ARA KWA MAADHIMISHO YA KIMATAIFA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA



Na Carlos Claudio, Dodoma.


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ametoa wito kwa wakazi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Kupinga Dawa za Kulevya Duniani, yatakayofanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia tarehe 24 hadi 26 Juni 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Jakaya Kikwete (JNICC), jijini Dodoma.


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Mhe. Senyamule amesema kuwa maadhimisho hayo ni ya muhimu kwa taifa kwani yanatoa fursa kwa wananchi kujifunza na kuelewa athari za dawa za kulevya pamoja na juhudi zinazofanywa na serikali na wadau katika kupambana na tatizo hilo linaloathiri nguvu kazi ya taifa, hususan vijana.


"Natoa wito kwa wakazi wa Dodoma na Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya ya kitaifa. Hii ni nafasi ya kipekee ya kupata elimu, kujifunza njia za kukabiliana na janga la dawa za kulevya na kusaidia wale waliokwishaathirika kurejea katika maisha ya kawaida," allmesema Mhe. Senyamule.


Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kuheshimiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.


Aidha, ameeleza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yataambatana na maonesho ya shughuli mbalimbali za udhibiti wa dawa za kulevya kutoka kwa taasisi na mashirika mbalimbali, pamoja na kongamano la vijana litakalojadili changamoto na fursa katika mapambano dhidi ya dawa hizo hatari.


“Mwezi wa Juni kila mwaka, dunia huadhimisha siku ya kupinga dawa za kulevya. Hapa Tanzania, kwa mwaka huu 2025, tunayo heshima kubwa kuwa wenyeji wa maadhimisho haya ya kitaifa ambayo ni sehemu ya kuhamasisha jamii na kutathmini hatua zilizofikiwa katika kupambana na matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya,” aliongeza.


Mhe. Senyamule amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji ushirikiano wa sekta zote na jamii kwa ujumla. Alitoa rai kwa wananchi kuwa mabalozi wa kutoa taarifa, kusaidia waathirika, na kuelimisha wengine juu ya madhara ya dawa hizo.





🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post