Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mwenyekiti na Muanzilishi wa Kariakoo Business Awards, Zakayo Shushu, amesema tuzo hizo zimeanzishwa kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa wafanyabiashara wa soko la Kariakoo katika kukuza uchumi wa taifa.
Akizungumza leo June 19,2025 jijini Dodoma baada ya kuitikia mwaliko rasmi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Shushu amesema kuwa walifika bungeni kushuhudia namna shughuli mbalimbali zinavyoendelea, ikiwemo mjadala wa bajeti ambao kwa kiasi kikubwa unawahusu wafanyabiashara.
“Kwa miaka mingi wafanyabiashara wa Kariakoo wamekuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa, lakini kwa bahati mbaya mchango wao haujawahi kutambuliwa ipasavyo. Kupitia tuzo hizi, tunaleta mabadiliko kwa kuwatambua rasmi wale wanaofanya kazi kwa ubunifu, uaminifu na bidii,” amesema Shushu.
Shushu amesema kuwa soko la Kariakoo ni miongoni mwa masoko makubwa barani Afrika, likiwa kitovu cha biashara na huduma mbalimbali. Kupitia tuzo hizo, wameanzisha jukwaa la kuwatambulisha wafanyabiashara mbele ya taifa na kimataifa, na kusaidia wateja pamoja na wadau mbalimbali kuwatambua kwa urahisi kutokana na ubora wa kazi na huduma zao.
Aidha, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kuunga mkono juhudi hizo kwa asilimia kubwa, sambamba na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo pamoja na Ushirika wa Masoko, kwa kutoa ushirikiano wa hali ya juu.
“Zaidi ya wafanyabiashara 1,500 wamejitokeza kushiriki katika tuzo zetu mwaka huu, jambo linaloonesha mwitikio mkubwa na hamasa ya kutaka kutambuliwa na kuthaminiwa,” ameongeza.
Shushu pia amewashukuru wadau mbalimbali wa maendeleo waliowaunga mkono, akiwemo Mamlaka ya Reli ya Tanzania (TRC) kupitia mradi wa reli ya kisasa – SGR, waliowapatia usafiri wa uhakika kufika Dodoma kushiriki tukio hilo muhimu.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.