Na Carlos Claudio, Dodoma.
Serikali imesema imeendelea kuweka mifumo bora ya fursa za kiuchumi,kijamii na katika uongozi kwa watu wenye ulemavu na makundi maalum nchini na kuwataka kuchangamkia fursa hizo kila zinapo tangazwa.
Hayo yameelezwa jijini hapa Dodoma na Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu ( Kazi,vijana,Ajira na wenye ulemavu) Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati alipomwakilisha Naibu Waziri mkuu na waziri wa Nishati Dkt. Doto Mashaka Biteko aliyetarajiwa kuwa mgeni rasm katika ufunguzi wa kongamano la kitaifa la watu wenye ulemavu.
Mhe.Ridhiwani amesema licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau katika kuhakikisha kundi la watumaalum wanapata haki sawa na watu wengine lakini baadhi yao wamekuwa na hali ya kutojiamini katika fursa hizo.
"Juhudi za serikali katika kukuza na kuendeleza ustawi wa watu wenye ulemavu tumezindua mpango kazi wa Taifa wa Haki na ustawi kwa watu wenye ualbino ( mwaka 2024/2025 hadi mwaka 2028/29) ili kuhakikisha jamii ya watu wenye ualbino wanaishi katika mazingira salama na kushiriki katika shughuli za kijamii,kisiasa,kiuchumi kwa utulivu na amani.
"Lakini pamoja na jitihada za serikali na wadau bado zipo changamoto zinazowakanili kundi hili la watu wenye ualbino kama baadhi yao kutokujiamini, hivyo serikali imeweka mifumo mizuri ya fursa za kiuchumi,kijamii na uongozi hivyo watu wenye ulemavu wajitokeze kuchangamkia fursa hizo,"amesema.
Pia amesema katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanaendelea kupata haki na ustawi wao serikali imekusudia kukamilisha mapitio ya sera ya Taifa ya huduma na maendeleo kwa watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 ili waweze kwendana na hali ya sasa pamoja na kukamilisha muongozo wa kitaifa wa viwango vya ufikivu kwa watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake Muasisi wa Ikupa Trust Fund Stella Ikupa, amesema kuwa licha ya juhudi za Serikali kuboresha huduma za afya, bado watu wenye ulemavu wanakumbwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa saidizi, miundombinu isiyokuwa rafiki, na uhaba wa watumishi wa afya waliopata mafunzo ya kuwahudumia kikamilifu.
"Changamoto hizi zimekuwa kikwazo kikubwa kwa watu wenye ulemavu katika kufurahia haki yao ya msingi ya kupata huduma bora za afya. Tunapojadili bima ya afya kwa wote, lazima tuhakikishe kuwa tunawaangalia watu wenye ulemavu kwa jicho la kipekee, kwa sababu mahitaji yao si sawa na ya watu wengine," amesema Bi. Ikupa.
Aidha, akigusia kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu, Bi. Ikupa amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika mchakato mzima wa siasa na demokrasia. Ametoa wito kwa vyama vya siasa, Tume ya Uchaguzi na vyombo vya habari kuhakikisha kunakuwepo na wakalimani wa lugha ya alama katika kampeni, mikutano ya hadhara na matangazo ya moja kwa moja ya kisiasa kupitia televisheni na majukwaa mengine ya habari.
“Ni muhimu kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wa kusikia wanapata taarifa sawa kama wananchi wengine. Hii ni sehemu ya haki ya kupata habari, ambayo ni msingi wa ushiriki kamili katika shughuli za kijamii na kisiasa,” amesisitiza.
Kwa upande mwingine, Bi. Ikupa amelipongeza shirika lake lililoandaa mkutano huo kwa udhamini wa PPRA kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapatiwa mahitaji yao muhimu, ikiwemo misaada ya vifaa saidizi, mafunzo ya kujitegemea, na elimu ya haki zao.
“Shirika hili limekuwa likifanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa kundi la watu wenye ulemavu linapaza sauti na linapewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa letu,” amesema.
Aidha ameishukuru Serikali kupitia PPRA kwa kutenga asilimia 30% ili makundi maalum yaweze kunufaika na mchakato wa manunuzi ya Umma.
Wito huu unakuja wakati Serikali ikiwa mbioni kuanza utekelezaji wa Sheria mpya ya Bima ya Afya kwa Wote, ambayo inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya afya bila ya kujali hali yake ya kiuchumi. Mashirika ya kiraia, wanaharakati wa haki za watu wenye ulemavu, na wadau wengine wanahimizwa kushirikiana kwa karibu na Serikali kuhakikisha kuwa mabadiliko hayo ya sera yanawajumuisha wote kwa usawa.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya udhibiti wa ununuzi wa umma Bw.Daniel Simba amesema jumla ya Makundi Maalum 335 yamekamilisha usajili na uhuishaji wa taarifa zao katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma (NeST) ambapo vijana ni vikundi 204 sawa na 61%, Wanawake ni Vikundi 108 sawa na 32%, Watu wenye Ulemavu ni vikundi 5 sawa na 2% na Wazee vikundi 18 sawa na 5%.
Aidha amesema tuzo za Mkataba zilizotolewa kwa watu wenye ulemavu ni 446 zenye Thamani ya Tsh. Bil 15.2 kati ya hizo Makundi ya Vijana yamepata tuzo za Mkataba 262 zenye thamani ya Bil 8.2 sawa na 54% , Makundi ya Wanawake yamepata tuzo za Mkataba 151 zenye thamani ya Bil 5.6 sawa na 37%, Makundi ya Watu wenye Ulemavu yamepata tuzo za Mkataba 14 zenye thamani ya Mil 174 sawa na 2% na Makundi ya Wazee yamepata tuzo za Mkataba 19 zenye thamani ya Mil 1.1 sawa na 7%.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.