Na Edward Winchislaus, Dodoma.
Jeshi la polisi mkoa wa Dodoma limewataka wafanyabiashara wa vyuma chakavu mkoani humo kutojihusisha na uhalifu wa miundombinu na mali za umma kutokana na baadhi yao kukamatwa kwa kununua mali za wizi.
Rai hiyo imetolewa leo Mei 12,2025 jijini hapa Dodoma na kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Dodoma RPC George Katabazi wakati wa mkutano wa jeshi la polisi na wafanyabiashara hao,ambapo RPC Katabazi amesema mkutano huo ulilenga kuleta ushirikiano wa pamoja kati ya jeshi hilo na wafanyabiashara wa vyuma chakavu ili kuweza kubaini na kuzuia uhalifu wa miundombinu.
RPC Katabazi amesema mkutano huo umekuja mara baada ya uwepo wa uhalifu wa miundombinu na mali mbalimbali ikiwemo milango ya nyumba iliyobomolewa pindi ujenzi wa nyumba ukiendelea na wahalifu hao kuuza mali hizo kama vyuma chakavu.
"Lengo kubwa la mkutano huu ni kuwa na ushirikiano kati ya jeshi la polisi na wafanyabiashara wa vyuma chakavu ili tuweze kuzuia na kubaini wezi wa miundombinu na mali za watu,sasa niwatake nyie wafanyabiashara wenye leseni za biashara hii mkemee wahalifu wote wa miundombinu.
"Biashara ya vyuma chakavu ni biashara halali lakini baadhi yenu mnafanya biashara hii kwa kununua mali za wizi na huku unakuwa unajua kuwa hii mali ni ya wizi imepatikana kwa njia isiyo halali lakini baadhi yenu mnanunua hizo mali na kuziita vyuma chakavu,pia hivyo vyuma chakavu muda mwingine unakuta siyo vyuma chakavu kwa uhalisia wake ila kwakuwa mtu kaiba kaleta mnanunua kama vyuma chakavu,hivyo leo tumeona tutoe Elimu na tuwaonye msijihusishe katika uhalifu huo,"amesema RPC Katabazi.
Amesema katika oparesheni iliyofanyika hivi karibuni ya kuwabaini wahalifu wanaojihusisha na wizi wa miundombinu na mali kisha kuziuza kama vyuma chakavu watu 21 tayari wamekamatwa kwa tuhuma hizo ambapo 11 kati yao wamefikishwa mahakamani kwaajili ya taratibu nyingine za kisheria.
"Katika oparesheni ya kukamata wahalifu wa miundombinu na mali za watu,tumewakamata watuhumiwa 21 ambapo 11 kati yao tumewafikisha mahakamani,mali hizi walizoziiba ni pamoja na Madirisha, Milango, Misalaba makaburini, miundombinu ikiwemo ya mifuniko ya kufunikia chemba za maji taka na vibao vya alama za barabarani .
"Maeneo yaliyokithiri kwa wizi mkubwa ni pamoja na Mkonze na Iyumbu kutokana na maeneo hayo kuendelea kupanuliwa kwa ujenzi na ukiangalia watuhumiwa 21 tuliyowakamata miongoni mwao ni Mafundi wa ujenzi nao wamekuwa wakishirikiana na wezi wa mali hizo,"amesema.
Aidha RPC. Katabazi amewataka wananchi wa mkoa wa Dodoma kufika kituoni hapo na kutambua mali zao zilizochukuliw kwa wizi ili hatua nyingine stahiki ziweze kuendelea huku akiwatadharisha wafanyabiashara wa bidhaa hiyo kuwa wazalendo wa miundimbinu mkoani humo.
Kwa upande wao wafanyabiara wa vyuma chakavu kwa nyakati tofauti wamelishukuru jeshi la polisi mkoa wa Dodoma kwa kuwapatia elimu ya kutojihusisha na uhalifu wa miundombinu pamoja na kutokununua mali zinazozaniwa kuwa za wizi huku wakiahidi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo wakati wote.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.