Serikali kupitia Wizara ya Madini imezitaka kampuni 95 za uchimbaji wa madini ambazo hazijaanza shughuli za uchimbaji licha ya kuwa na leseni halali, kujieleza ndani ya siku 30 kuanzia Mei 6, 2025, au vinginevyo zitafutiwa leseni zao kwa mujibu wa sheria.
Agizo hilo limetolewa siku ya Jumanne na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, mkoani Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya usimamizi wa sekta hiyo.
"Kama wana hoja walete majibu yao, tuyahakiki tukijiridhisha na hoja zao tutawaondolea makatazo kama hawana hoja tutawafutia leseni zao kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura 123 ya utoaji na ufutaji wa leseni za madini na uchimbaji kifungu cha 63 na Kanuni zake, ambacho kinaeleza ukipewa leseni unapaswa uanze kazi ndani ya miezi 18", amesema Mavunde.
Kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura ya 123, kifungu cha 63, kampuni yoyote inapopewa leseni ya uchimbaji, ina wajibu wa kuanza kazi ndani ya miezi 18 au kutoa sababu zitakazoridhiwa na Tume ya Madini.
Mavunde amesema kampuni hizo nyingi ni za wachimbaji wa kati na wakubwa waliopatiwa leseni kati ya mwaka 2011 hadi sasa, lakini bado hawajaanza kazi yoyote ya uchimbaji, jambo ambalo linaathiri maendeleo ya sekta hiyo na mapato ya taifa.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.