Na Mwandishi wetu Dodoma.
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali inatarajia kuadhimisha Siku ya Punda Kitaifa Mei 17, 2025 katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma ili kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kumhifadhi na kumtunza mnyama punda.
Akizungumza leo (15.05.2025) kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ndogo za wizara zilizopo jengo la NBC jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo wa ofisi hiyo Dkt. Benezeth Lutege, amesema maadhimisho hayo yana kauli mbiu isemayo “Dhamira ya Afrika Katika Kuhifadhi Punda Sasa na Siku Zijazo”.
Aidha, Dkt. Lutege amesema serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha mnyama punda analindwa, zikiwemo za kusitisha shughuli za kumchinja mnyama huyo pamoja na ununuzi wa ngozi yake.
Pia, amesema serikali inaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau katika masuala ya ustawi wa wanyama na kuhakikisha biashara ya nyama na ngozi za punda inakomeshwa.
Dkt. Lutege ametoa wito kwa wananchi kushiriki katika maadhimisho hayo kuanzia Mei 16, 2025 yatakayoambatana na maonesho ya elimu kuhusu mnyama punda pamoja na huduma za kitabibu za mnyama huyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kiafrika ya Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii (INADES – Formation, Tanzania) Bw. Mbarwa Kivuyo amesema sambamba na maadhimisho hayo taasisi imeandaa kitabu maalum chenye lugha ya kiswahili kitakachoitwa “Punda Wangu Maisha Yangu” na kuzinduliwa siku hiyo kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii kuhusu utunzaji wa mnyama punda.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.