BENKI YA DUNIA KUJENGA KM 100 ZA BARABARA ZA LAMI RUANGWA


Waziri Mkuu wa Tanzania na Mbunge wa Ruangwa Mkoani Lindi Kassim Majaliwa ameeleza kuwa Benki ya Dunia imetoa ufadhili wa ujenzi wa kilomita 100 za barabara za kiwango cha lami Wilayani Ruangwa ambapo kukamilika kwake kutachochea na kusisimua uchumi wa Wilaya hiyo na kuchagiza maendeleo kwa wananchi.


Majaliwa ameyasema hayo Jumamosi Wilayani Ruangwa, alipokutana na Wajumbe wa Jumuiya za CCM na Wazee wa Wilaya ya Ruangwa, akieleza kuwa ujenzi wa barabara hizo utaenda sambamba na ufungaji wa taa pembezoni mwa barabara za vijiji vya pembezoni mwa Barabara kuu ya Ruangwa-Nachingwea.


Majaliwa amezitaja barabara zitakazojengwa kwa ufadhili huo wa Benki ya Dunia kuwa ni Barabara ya Mandawa-Mkalanga (Km 16), Nandenje-Kwachani (Km.10), Nangwego-Nankatila (Km.24, Ruangwa-Nangurugai (Km.26) na barabara ya Nandagala-Matankini (Km.24) ambapo tayari wataalamu wa tathimini ya fidia wameshaanza kufanya chambuzi kujua kuhusu fidia kwa watakaoathirika na ujenzi huo.


Waziri Mkuu Majaliwa amebainisha pia kwamba serikali inajenga barabara za Mjini kwa kiwango cha lami zikiwemo Barabara za Chimbila- Ng'au mpaka Mahakamani, Lichonyo- Majaliwa Complex-Ruangwa Girls pamoja na barabara nyinginezo, mpango ukiwa ni kuiunganisha Ruangwa na wilaya zote za pembezoni.


Amezungumzia huduma za maji na umeme wilayani Ruangwa, akibainisha kuwa kwasasa vijiji vyote vya Ruangwa vina huduma ya umeme na kazi kubwa kwasasa ni usambazaji wa huduma hiyo kwa ngazi ya vitongoji, huku pia serikali ikiendelea na ujenzi wa mradi mkubwa wa maji kwa vijji 54 vya Ruangwa na Nachingwea, akieleza kuwa ana imani kuwa miradi yote itakamilika kama ilivyokusudiwa.


🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post