ZELENSKY ANAWEZA KUIACHIA CRIMEA KWA URUSI- TRUMP



Rais wa Marekani Donald Trump amedai kuwa anaamini Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky yuko tayari kuachana na eneo la Crimea kwa Urusi kama sehemu ya makubaliano ya amani licha ya msimamo wa muda mrefu wa Kyiv wa kukataa pendekezo lolote la aina hiyo.


Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kurejea kutoka Vatican, ambako alikutana kwa kifupi na Zelensky kabla ya mazishi ya Papa Francis, Trump alisema: "Nadhani hivyo," alipoulizwa iwapo anaamini Zelensky yuko tayari kuliachilia Crimea.


Katika mazungumzo hayo, Trump pia alimshawishi Rais wa Urusi Vladimir Putin kuacha mashambulizi hidi ya Ukraine na badala yake "kuketi chini na kusaini makubaliano" ambayo, kwa mujibu wake, yanaweza kufikiwa ndani ya kipindi kifupi cha wiki mbili.


Trump alisema kuwa mkutano wake na Zelensky "ulienda vizuri", ingawa suala la Crimea lilijadiliwa "kwa ufupi sana".


Aliongeza kuwa aliona Zelensky akiwa mtulivu zaidi ikilinganishwa na mkutano wao wa awali White House Februari mwaka huu, ambao ulionekana kuwa na mvutano wa hadharani.


Kwa muda mrefu, Ukraine imekataa kukubali makubaliano yoyote ya amani yanayohusisha kupoteza sehemu ya ardhi yake, ikisema

kuwa suala la mipaka ya kitaifa halipaswi kujadiliwa hadi pale usitishaji wa mapigano utakapoafikiwa.


Kwa sasa, Zelensky wala Putin hawajato majibu ya hadharani kuhusu maoni haya ya hivi karibuni kutoka kwa Trump.


Mapema Jumapili, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius aliionya Ukraine dhidi ya kukubali mapendekezo yanayohusisha kupoteza ardhi kwa lengo la kufikia usitishaji wa mapigano.


Akihojiwa na shirika la utangazaji la ARD la Ujerumani, Pistorius alisema: "Kyiv haipaswi kufikia pendekezo la hivi punde la rais wa Marekani, ambalo litalinganishwa na kujisalimisha."


Hata hivyo, Waziri huyo alikiri kwamba Ukraine inaweza, mwishowe, kulazimika kuachana na baadhi ya maeneo ili kufikia suluhu ya kudumu ya vita hiyo.


🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post