Na Edward Winchislaus, Dodoma.
Waziri wa nchi,Ofisi ya waziri mkuu, kazi, Vijana ,Ajira na wenye ulemavu Mhe.Ridhiwani Jakaya Kikwete amesema matumizi ya Teknolojia na akili unde katika nyanja ya usalama na Afya kazini ni nyenzo muhimu hivyo hainabudi kutumiwa kwa usahihi pamoja na kuweka mbele usalama wa wafanyakazi na haki za binadamu ili kupunguza hatari za moja kwa moja kwa wafanyakazi hao.
Hayo ameyasema leo Aprili 23,2025 wakati akizungumza na waandishi wa Habari jijini hapa Dodoma kuhusu maadhimisho ya siku ya kimataifa ya usalama na Afya mahali pa kazi yatakayofanyika Aprili 28 mwaka huu Mkoani Singida.
Mhe.Kikwete amesema licha ya Teknolojia kupunguza hatari za moja kwa moja kwa wafanyakazi lakini imeongeza vihatarishi vipya kama vile uchovu wa akili,matatizo ya macho na matatizo ya kiafya yatokanayo na kukaa kwa muda mrefu.
"Siku ya usalama na Afya mahali pa kazi Duniani ilianza kuadhimishwa mwaka 1996 na shirikisho la vyama ya wafanyakazi Duniani huko jijini New York Nchini marekani,na hapa Nchini siku hii ilianza kuadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004,tangu mwaka huo tumekuwa tukiadhimisha na mwaka huu maadhimisho haya yatafanyika kwa mara ya 21.
"Katika nyanja ya usalama na Afya kazini tunahitaji kuhakikisha kuwa matumizi ya Teknolojia hizi yanaambatana na kuwalinda wafanyakazi hususani na vihatarishi vipya ikiwemo kufanya mapitio ya kanuni za usalama na Afya kazini,mafunzo sahihi,na ufuatiliaji endelevu maana utumiaji wa Teknolojia na akili mnemba si adui yetu bali ni nyenzo yenye nguvu kubwa,"amesema.
Pia amewahimiza waajiri nchini kuendelea kufanya usajili wa sehemu za kazi ambapo amesema lengo ni kuyatambua maeneo yao na kuendelea kuyasimamia pamoja na kuyapa miongozo muhimu itakayowezesha kuboresha mazingira ya kazi nchini.
"Tunapenda kutoa wito kwa waajili wote kuhakikisha kwamba wanasajili maeneo yao ya kazi OSHA pamoja na kuendelea kutekeleza taratibu mbalimbali za usalama na Afya kwa mujibu wa sheria Na:5 ya usalama na Afya mahali pa kazi ya mwaka 2003,unaweza jisajili na OSHA ukiwa mahali popote bila ya kufunga safari kuja OSHA,kupitia mtandao wa Workplace Information Management System ( WIMS),"amesema Kikwete.
Aidha amesema katika kuelekea maadhimisho hayo serikali kwa kushirikiana na wadau wake wa utatu wanaendelea na kampeni maalum ya uhamasishaji kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo mafunzo ya usalama na Afya miongoni mwa makundi mbalimbali kama wajasiriamali wadogo na watu wenye ulemavu.
Vilevile amebainisha kuwa shughuli nyinginezo ni uwepo wa Bonanza la michezo miongoni mwa washiriki wa maonesho na wananchi kwa ujumla pamoja na kliniki ya uchunguzi wa Afya za wafanyakazi.
"Kampeni hii ya mafunzo tumekuwa tukiifanya kwa lengo la kuyafikia makundi yote hususani makundi ambayo bado mwamko wa masuala ya usalama na Afya yapo chini kidogo,maonesho ya usalama na Afya mahali pa kazi ambayo yatawakutanisha wamiliki/ wasimamizi wa sehemu za kazi na wadau wengine ili kutoa elimu kwa umma na kubadilishana uzoefu miongoni mwao juu ya masuala ya usalama na Afya mahali pa kazi,"amesema.
Hata hivyo maadhimisho ya siku ya usalama mahali pa kazi Tanzania mwaka 2025 yataenda sambamba na kauli mbiu isemayo "Nafasi ya akili mnemba na Teknolojia za kidijitali katika mapinduzi ya usalama na Afya kazini"na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa nchi,Ofisi ya Waziri mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye ulemavu Mhe.Ridhiwani Jakaya Kikwete.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.