"Serikali iliandaa na kushiriki Mutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Nishati (African Heads of States Energy Summit) uliofanyika tarehe 27-28 Januari, 2025 Jijini Dar es salaam.
Pamoja na mambo mengine, kupitia mutano huo Mpango wa Kitaifa wa Nishati wa Tanzania (National Energy Compact) ulizindulia, ambao unalenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2030 kutoka cha sasa cha asilimia 78.4; kuongeza kasi ya kuunganisha umeme nchini hadi kufikia asilimia 75 katika kipindi hicho kutoka asilimia 46 za sasa; kuongeza kiwango cha matumizi ya nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 6.9 ya mwaka 2021 hadi asilimia 75 ifikapo mwaka 2030; na kuongeza mchango wa sekta binafsi katika Sekta ya Nishati kwa kiasi cha Dola za Marekani bilioni 4.39 sawa na takriban Shilingi trilioni 11.73 ifikapo mwaka 2030.
Mhe. Spika kupitia mutano huo, Wakuu wa Nchi za Afrika walisaini Azimio la utekelezaji wa Mpango huo (Dar es Salaam Declaration by the African Heads of States Energy Summit), ikiwa ni makubaliano ya pamoja ya Wakuu hao ya kuunganisha nguvu na jitihada za pamoja za kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha zitakazowezesha upatikanaji wa huduma ya umeme wa uhakika, endelevu na gharama nafuu kwa watu milioni 300 katika Bara la Afrika ifikapo 2030.
Nitumie fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu, kumpongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Nishati Afrika (Mission 300) kwa Mwaka 2025.
Aidha, Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini yake inakamilisha uandaaji wa Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Nishati (National Energy Compact) ambao utekelezaji wake utaanza Mwaka 2025/26.
"Serikali chini ya uratibu wa Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inaendelea na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 - 2034) uliozinduliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 08 Mei 2024. Lengo la Mkakati huo ni kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Manufaa ya utekelezaji wa Mkakati huu ni pamoja na kuwaepusha wananchi na athari za kiafya zitokanazo na matumizi ya nishati zisizo safi za kupikia na kukabiliana na uharibifu wa mazingira
unaotokana na matumizi ya nishati zisizo safi za kupikia.
Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa nishati safi ya kupikia pamoja na kuwezesha ujenzi wa
miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika Taasisi za Umma na binafsi zinazohudumia zaidi ya watu 100 kwa siku, ikiwemo Jeshi la Magereza, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Shule za Sekondari.
Aidha, zoezi la kusambaza mitungi 452,445 ya gesi ya kupikia (LPG) kwa bei ya punguzo la hadi asilimia 50 liliendelea, na kupitia programu hii jumla ya mitungi 154,224 imesambazwa hadi kufikia Aprili 2025."-@biteko Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa nishati akisoma bajeti ya Wizara ya nishati kwa mwaka 2025/26.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.