Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameeleza kuwa hadi kufikia Juni 30, 2024, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) inadaiwa jumla ya Shilingi bilioni 595, ambapo kati ya hizo, Shilingi bilioni 369.13 ni madai kutoka taasisi za Serikali.
Ripoti hiyo ya CAG kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imebainisha kuwa fedha hizo zinahusiana moja kwa moja na malipo ya ukodishaji wa ndege kutoka Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), kupitia masharti nafuu yaliyowekwa kwenye mikataba ya ukodishaji.
Hata hivyo, ucheleweshaji wa ulipaji wa madeni hayo umetajwa kuchangiwa na mapato natitu ya kampuni kutoka vyanzo vya ndani, pamoja na changamoto Katika usimamizi wa mkataba wa ukodishaji.
Aidha, ripoti imeeleza kuwa Kampuni ya Ndege Tanzania imeshindwa kulipa kodi na tozo za akiba ya matengenezo ya ndege kwa kipindi cha miaka sita mfululizo, hali iliyosababisha deni hilo kuongezeka kutoka Shilingi bilioni 27.89 mnamo Juni 30, 2018, hadi kufikia Shilingi bilioni 369.13 mwaka 2024.
CAG ameonya kuwa kiasi hicho kinatokana na gharama kubwa za vendeshaji na matengenezo ya ndege, pamoja na hasara ya kifedha ambayo kampuni hiyo imekuwa ikiipata kwa miaka sita mfululizo.
Hali hiyo imeongeza migo wa kifedha kwa Shirika, hali inayohatarisha ustawi wake wa muda mrefu.
Katika mapendekezo yake, CAG ameshauri ATCL na Wakala wa Ndege wa Serikali kukaa pamoja na kukubaliana mpango wa malipo wa kodi na tozo hizo.
Mpango huo unapendekezwa kujumuisha urekebishaji wa deni, kuongeza muda wa ulipaji, na kupunguza kiwango cha tozo za kila mwezi ili kuwezesha kampuni hiyo kumudu mzigo wa madeni na kujiendesha kwa ufanisi zaidi.