Na Fedrick Mbaruku
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameitaka Bodi ya Mfuko wa Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Wafanyakazi wa serikalini,PSSSF, Menejimenti na Watumishi wote kuanzisha mfuko maalumu kwa Wastaafu ili kuwaepusha na usumbufu wa kutapeliwa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Agosti 12, 2023 wakati wa maadhimisho ya miaka mitano ya mfuko huo na uzinduzi wa mfumo wa dijitali yaliyofanyika katika Ukumbi wa PSSSF Jijini Dodoma.
Amesema watendaji PSSSF wanatakiwa kuhakikisha wanayatekeleza vema majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ili kulinda mafanikio yaliyopatikana na kuendeleza rekodi zaidi.
“Wanachama wa mfuko mlioko kazini wekeni utaratibu wa kutembelea mifuko yenu ili kuona kama taarifa zenu zikosawa.
“Taasisi za serikali zihakikishe mifumo ambayo tunaizindua wataalamu wa Tehama nendeni mbali izungumze hii ndio kazi ambayo sasa tunaanza nayo kuhakikisha kwamba mifumo mbele ya serikali inazungumza yote,” amesema.
Waziri Mkuu Pia amempongeza mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge kwa kuendelea kuishauri mifuko ya hifadhi ya jamii, kusimamia na kuonesha changamoto zinazobainishwa na wananchi na wadau wastaafu nchini.
Aidha Waziri Mkuu amesema ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na mifuko ya jamii ukiwemo mfuko wa PSSSF itaendelea kusikiliza,kupokea na kutekeleza ushauri unaotolewa na taasisi hiyo.