Na Minaeli Mapala
Ni familia ngapi zinaweza kumudu gharama za kuwapeleka Watoto wao shule katika kipindi hiki kifupi tokea matokeo ya kidato cha nne yametoka ambapo ikifika Agosti 14 wanatakiwa kuwasili shuleni wakiwa na vifaa vilivyokamilika ikiwemo pesa yakujikimu.
Je! ni sawa kwa Wizara ya elimu kutoa muda wa mwezi mmoja kwa mwanafunzi kuripoti shule aliyopangiwa tangu ilipotolewa orodha ya waliochaguliwa Juni 11 na kumtaka mwanafunzi kuripoti shule ifikapo Agosti 14?
Sote tunajua hali zetu sisi watanzania ambapo ukitolea mfano tu mjasiriamali mdogo kipato chake kwa mwaka hakizidi millioni nne lakini ukiachana na kusomesha anamajukumu mengine anatakiwa kuyafanikisha ili maisha yake yaweze kwenda.? Mara nyingi huwa tunaomba muda katika utafutaji sasa kwa hili mdau mwenzangu unadhani limekaaje wazazi wataweza kweli?
Katika asilimia 69% ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu ifahamike kuwa wanatoka katika familia zenye uchumi tofauti tofauti na katika familia zetu za kitanzania nyingi zina vipato vya chini, swali kwenu Wizara ya elimu mnadhani ni sahihi kutoa orodha ya wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na kidato cha tano wakati huu ilihali matokeo yametoka tangu Januari?
Kulingana na takwimu ambazo huwa zinafanywa mara kwa mara na baadhi ya mashirika kama Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuhusu uchumi wamtanzania mmoja mmoja tunaona kwamba ili maisha ya mtanzania yaweze kuendelea bila shida yanahitaji maandalizi ndio maana yanapotokea matukio ya ghafla kama magojwa au hata vifo mara nyingi uchumi wa muhusika huwa unayumba hivyo kwa kulijua hilo kwanini serikali haikuona haja yakuwapa muda wahusika ili kuwasaidia kujiandaa?
Ukiangalia kwa jicho la ndani utagundua kuna mambo mengi yamesitishwa ili kumwezesha mtoto kwenda shule ambapo kama serikali ingepanga mapema shule basi mzazi asingehangaika kutafuta mkopo au hata kuuza kitu kwa ghafla ili kumfanya mtoto asome najua unatambua kutokana na hili hadi sasa madeni ni mengi sana huko mtaani.
Chaajabu zaidi wamiliki wa mikopo umiza na kausha damu ndio hutumia fursa kuweza kumkandamiza mtanzania ambae anapambania ndoto ya mtoto wake, tutaona mengi baada ya miezi mitatu mbele vile wazazi wakiwajibishwa kulipa mkopo, kunyang’anywa nyumba na vitu vya thamani wanavyomiliki ili aweze kulipa deni ambalo kama serikali ingemuandaa mapema basi asingekopa.
Miaka kadhaa iliyopita Wizara ya Elimu ilikua ikitoa matokeo kwa wakati na orodha ya kujiunga na kidato cha tano mapema hali ambayo ilikua inasaidia familia nyingi kujipanga na kufanya maandalizi hayo kwa wakati,Wizara ya elimu haioni kama kuna manufaa kutoa orodha hiyo mapema ya wanafunzi.
Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania imekuwa na kampeni mbalimbali za kutoa michango yake katika elimu kubwa ni elimu bure ambapo serikali imeongoza elimu kuwa bure hadi kidato cha sita.
Ni jambo la faraja kwa watanzania wengi wanapofikia elimu bure hususani familia zenye kipato cha chini ambao hawana uwezo wa kusomesha watoto wao katika shule na kulipia gharama za juu.
Ninafahamu fika katika familia zetu za kitanzania kuna watu wenye vipato vya juu ambao hawahitaji hata maandalizi yoyote ya kujiandaa lakini pia ifahamike kuwa kuna familia zile zenye kipato cha chini na wanahitaji muda wa kutosha katika maandalizi ili kumuwezesha mwanafunzi kuripoti shuleni.
Kila mahali kunapokuwa na uongozi lazima kuwe na kanuni na sheria zinazowaongoza watu,Je wizara ya elimu kwa kipindi chote hiki kulingana na ratiba au taratibu zao za utoaji orodha za wanafunzi kujiunga kidato cha tano haioni ni vema kufanya mabadiliko katika hili.
Wazazi pia wanapaswa kujiandaa mapema pindi watoto wanapokua wamefaulu wakati wakisubri kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano kwani kwa wale wenye kipato cha chini wanapaswa kujiandaa mapema kuhakikisha fedha ya sare ya shule inakuewepo pamoja na madaftari.
Nipende kushauri Wizara ya elimu irejelee kipindi cha miaka kadhaa ya nyuma iliyopita kama wanaweza kutoa matokeo mapema ya wanafunzi kuanzia januari iandae orodha hiyo mapema ya wanafunzi hii itasaidia familia nyingi zenye kipato cha chini kufanikiwa kuwapeleka wanafunzi kuripoti kwa wakati
Nashauri Serikali kupitia Elimu bure ibaini wanafunzi wenye changamoto za kiuchumi na kuwaondolea gharama zote mahususi kwa wanafunzi anapojiunga na kidato cha tano ikiwemo rimu, majembe, fagio, fekeo, nguo za michezo(tracksuit)na kuwahimiza watafute sare za shule tu na kuripoti sababu vifaa hivyo vimekua vikiwafanya wazazi kushindwa kuwapeleka shule kwa wakati.
Wizara ya elimu iwapangie wanafunzi shule katika mikoa na wilaya za karibu na wanakotoka kulingana na shule za sekondari ambazo wamesoma ili kupunguza gharama za usafiri kwa mtoto na itasaidia wazazi kutokua na maandalizi mengi.